Jubilee imesaliti maskini kwa kupuuza maafa ya pombe

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Thursday, May 8  2014 at  11:41

Kwa Muhtasari

Hatua ambazo zinachukuliwa na serikali hii siku baada ya siku, zinabainisha kwamba hamna tofauti kubwa sana kati ya serikali hii na serikali za awali. Ni serikali ya mabwanyenye ambao lengo lao ni kuendelea kujivunia utajiri wao na mali yao.

 

WAKATI wa kampeni na hata wakati wa kutwaa mamlaka mwaka jana, muungano wa Jubilee ulijipendekeza kwa raia kama muungano wa kutetea maslahi ya maskini.

Lakini hatua ambazo zinachukuliwa na serikali hii siku baada ya siku, zinabainisha kwamba hamna tofauti kubwa sana kati ya serikali hii na serikali za awali.

Ni serikali ya mabwanyenye ambao lengo lao ni kuendelea kujivunia utajiri wao na mali yao. Uhusiano wa maskini na serikali ulifika kikomo baada yao kupiga kura Machi 4 mwaka jana na hali isipobadilika, watahitajika tena Agosti 2017.

Tukio linaloashiria ukweli wa haya ni maafa ambayo yamekumba wakazi wa kaunti za Embu, Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nairobi, Kitui na Makueni ambapo watu zaidi ya 80 walifariki baada ya kubugia pombe haramu.

Kwa siku mbili, viongozi wakuu serikalini walikuwa kimya, hali tofauti kabisa na ilivyokuwa shambulio la kigaidi lilipotekelezwa kwenye duka la jumla la Westgate ambapo jamaa za Rais Kenyatta waliathiriwa.

Mashambulio ya kigaidi yanapotekelezwa mijini na mahotelini, ambapo maslahi ya matajiri yanawekwa hatarini, serikali imekuwa mstari wa mbele kujitokeza na kulaani mashambulio hayo na kuapa kwamba itakabiliana vikali na wahusika. Ajali za barabarani pia kwa kiwango fulani zimechukuliwa kwa uzito.

Lakini maskini waliokufa kwa sababu ya kunywa pombe ya Sh30? Walikuwa wanasumbuliwa na nini? Mbona hawakunywa pombe na bia rasmi zinazouzwa kwenye baa ambapo hawangehatarisha maisha? Hao ni watu waliojitakia msiba! Haya yanaonekana kuwa mawazo ya serikali, ambayo pia nimeyasikia kutoka kwa marafiki zangu. Wanachosahau ni kwamba walalahoi hawa wangetamani sana kunywa divai na bia nyingine ghali lakini uwezo hawana.

Aidha, hawakunywa Wings, Kavuthuria, Countryman na Sacramento wakijua kwamba zilikuwa na sumu. Walikuwa wamewaamini watawala kwamba wangehakikisha viwango vya kuandaa pombe hizi vinafuatwa na hivyo kuwaepusha mauti.

Machifu

Wengi wa walevi hawa pia hunywa kukimbia upweke nyumbani labda kwa sababu hawana runinga au stima ya kuwawezesha kupitisha muda wao wa jioni baada ya kazi, au kazi inapokosekana. Binadamu hawezi akakaa kwenye giza chumbani akajitumbuiza, lazima atangamane na wenzake.

Jambo linalosikitisha zaidi ni kwamba 'Hustler Nambari Moja’ Naibu Rais William Ruto ndiye aliyekuwa ameachiwa usukani wakati huu, lakini hawezi kukumbuka 'Mahustler’ wenzake.

Jambo linaloudhi ni kwamba maafisa wa serikali wa viwango vya chini, machifu na manaibu wao, ambao wengi ni walalahoi pia ndio waliofutwa. Vigogo serikalini wanaendelea kunywa mvinyo na kula vinono! Maskini ajue hana lake.

pmwai@ke.nationmedia.com