Uhuru, kujipendekeza kwa umma pekee hakutoshi

Na Peter Mwai

Imepakiwa - Friday, May 29  2015 at  16:15

Kwa Muhtasari

Vitendo vya Rais Kenyatta kujinyenyekeza na kutangamana na watu vingelitumiwa kama kigezo cha utendakazi wa Rais, basi angeibuka nambari wani. Lakini ukweli ni kwamba haya huwa ya kufurahisha macho na fikira za watu kwani baada ya hapo, wananchi hurudi kukumbana na maisha magumu na shida nyingine za dunia.

 

RAIS Uhuru Kenyatta alichaguliwa na Wakenya kuongoza taifa hili miaka miwili iliyopita kutokana na sifa zake za kutaka kutangamana na watu.

Licha ya kuzaliwa ikuluni na kutangamana na watu wenye ushawishi mkubwa nchini, ni mtu anayependa sana kujihusisha na wananchi wa kawaida.

Katita UhuRuto, kama ulivyojulikana ushirikiano wake na Naibu wake William Ruto wakati huo akiwa mgombea mwenza, wapiga kura waliona 'vijana’ wanaoweza kuwatega sikio na kusikia vilio vya wananchi.

Wengi wamedai Rais Kenyatta huwa anaiga Rais wa Marekani Barack Obama ambaye amejulikana sana kwa kutangamana sana na watu na kuwapa walinzi wake kazi ngumu.

Ninaamini hii ni sifa yake asili na wala hamuigi Obama.

Majuzi tu alikuwa muungwana kiasi cha kuwashikia mwavuli wanawake wawili wakitoka kwenye ndege baada ya mvua kunyesha wakiwasili ikuluni White House.

Hapa nyumbani, Rais alimetenda mengi. Amekaribisha watu wengi sana ikulu, wakiwemo watoto, na kwa sasa makao makuu hayo ya uongozi ambayo watu walizoea kuyatazama tu kwa mbali yamekuwa ya wananchi.

Mwaka uliopita, alipigwa picha akiwa pamoja na Ruto wakila nyama choma eneo la kawaida Kajiado. Juzi, alifika kwenye kioski na kununua soda kisha akainywa kama mwananchi wa kawaida jambo lililovutia wengi.

Haya yote yangelitumiwa kama kigezo cha utendakazi wa Rais, basi Uhuru angeibuka nambari wani. Lakini ukweli ni kwamba haya huwa ya kufurahisha macho na fikira za watu kwani baada ya hapo, wananchi hurudi kukumbana na maisha magumu na shida nyingine za dunia.

Sikushangaa nilipoona kwenye utafiti wa Ipsos-Synovate kwamba umaarufu wake umeshuka kutoka asilimia 67 Novemba hadi asilimia 48 kufikia Aprili mwaka huu.

Hizi ni dalili kwamba wananchi hawaridhishwi na utendakazi wa serikali yake. Kuna mambo mengi ambayo yanawatatiza wananchi lakini Rais haonekani kujishughulisha nayo.

Kutojali

Mwanzo ni tatizo la usalama. Wananchi wanauawa kama nzi kila pembe ya nchi. Polisi pia hawajasazwa. Alipokuwa akinywa soda Machakos, kumbukumbu za kuhangaishwa kwa maafisa wa polisi na Al-Shabaab Yumbis, Garissa mapema wiki hii zilikuwa bado akilini mwa watu.

Gharama ya maisha pia imepanda pakubwa lakini serikali yake haionekani kujali.

Mengi anayotangaza hadharani hayatekelezwi na maafisa walio mashinani. Mfano tangazo lake kwamba bei ya kuwekea watu stima ishuke hadi Sh15,000 kutoka Sh35,000. Hafahamu kuwa hata kuitishwa hizo Sh35,000 kwa wengi imekuwa ndoto.

Majuzi pia alitoa agizo kwa makurutu wafike Kiganjo, lakini siku moja baadaye Serikali ikawafukuza kituoni.

Na vita dhidi ya ufisadi nani ana matumaini? Kushughulikia haya ni bora kuliko kunywa soda!

pmwai@ke.nationmedia.com