Kifo kimetupoka tena johari adhimu wa Fasihi ya Kiingereza Profesa Chris Lukorito Wanjala

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, October 17  2018 at  07:38

Kwa Muhtasari

Prof Chris Lukorito Wanjala ameenda njia ya marahaba.

 

KIFO kimetupiga pute msomi mwengine wa kutajika. Prof Chris Lukorito Wanjala ameenda njia ya marahaba.

Tanzia ya kifo chake imenilipukia Jumatatu mchana kama bomu la Hiroshima na Nagasaki. Nimeshtuka sana.

Nilikuwa na Prof Wanjala katika hafla ya kumuenzi msomi mwenzake mkongwe kutoka Uganda, Prof Augustine Lwanga Bukenya katika jengo moja liliko kwenye barabara ya Waiyaki Way Nairobi mwezi uliopita.

Niliandika katika safu hii furaha niliyokuwa nayo kwa kutangamana na magwiji wa fasihi katika hafla hiyo, magwiji waliochangia bila kujua azma yangu ya kuwa mwandishi wa kubuni na mhakiki wa fasihi na utamaduni.

Naam Chris Wanjala alikuwa miongoni, si tu wa waliohudhuria hafla hiyo, bali pia mwasilishaji alitukomoa kutoka kwa maruerue ya ujinga kwa kutupasha mambo ya kina kuhusu historia ya fasihi Afrika Mashariki. Alizungumza mengi kuhusu mabadiliko ya idara ya Kiingereza hadi idara ya Fasihi katika Chuo Kikuu cha Nairobi wakati azma ya wasomi Wafrika kutaka kujinasua kutoka kwa mikatale ya usomi wa kikoloni. Alimtaja Ngugi wa Thiong’o, Micere Mugo, Awour Anyumba, na Augustine Bukenya ( Austine Bukenya) kuwa miongoni mwa wasomi jasiri walioleta mapinduzi katika ufundishwaji, ujifundishaji na ufundishaji wa fasihi katika vyuo vyetu.

Niliemewa na kufarijika kwa uelewa wake wenye uketo wa historia hiyo ambayo nahofia huenda itakwenda naye. Nahofia kwa vile miaka kumi iliyopita alinitajia kwamba anapanga kuandika tawasifu ya maisha yake. Hiyo bila shaka ingekuwa na mengi ya kutujuza kuhusu msomi huyu mahiri aliyetokea sehemu ya Chesamisi, Bungoma. Ila hadi kufikia kifo chake sina habari kama tawasifu hiyo iliyo hazina kubwa ilikwisha kamilika ili kutuondoa ukungu machoni.

Prof Wanjala alikuwa miongoni mwa wahakiki waliobobea. Mbali na kuhariri diwani ya hadithi fupi ya Memories we Lost, ambayo inatahiniwa katika mtaala wa shule za sekondari, aliandika pia Season of Harvest miongoni mwa vitabu vingine. Ila kama Memories we Lost kinaakisi mtindo wetu wa kusahau mambo yaliyo muhimu kwetu, nahofia kwamba huenda mchango wa msomi huyu ukaishia katika kutupwa katika kaburi la sahau.

Mimi niliwahi kumtolea changamoto Chris Wanjala kwa kile kilichokiona kuwa mapuuza yake kwa fasihi ya Kiswahili. Kauli hiyo nilimtolea alipokuwa anatoa hotuba yake kuu katika Chuo Kikuu cha Nairobi nadhani mwaka 2000. Punde si punde aliniarifu kwamba sio tu  kwamba anasoma fasihi ya Kiswahili bali pia anaifundisha hata kitabu changu cha Nasikia Sauti ya Mama. Nilifarijika mno kwa unyenyekevu wake. Kwa hakika alizingatia hoja niliyoitoa katika unyonge na ulimbukeni wangu.

Nasikitika kwamba wakati alipolumbana na David Mailu na Taban Li Lyongo katika ukumbi mmoja chuoni kwake 2013, hakuna hata kamera moja ya video iliyounasa mdahalo huo wa kihistoria. Hapa tena nikang’amua kuhusu mtindo wetu wa kutupa mashujaa wetu katika shimo la sahau.

Machozi yananitoka njia mbilimbili.

Prof. Ken Walibora ni msomi wa fasihi, mwanahabari na mwandishi mtajika katika ulimwengu wa Kiswahili