Ni kawaida Wakenya, Watanzania kuwania nafasi za kufunza Kiswahili nje ya nchi

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, October 3  2018 at  09:51

Kwa Muhtasari

  • Wakenya wanaotea nafasi za kwenda kufundisha Kiswahili Afrika Kusini

  • Watanzania wanaotea nafasi za ajira kwenda kufundisha Kiswahili Afrika Kusini

 

HIVI majuzi nilihojiwa na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) Sarah Kimani.

Kama umekuwa ukifuatia mambo vizuri utaelewa kwamba Afrika imekuwa inagonga vichwa vya habari, sio kwa sababu ya kuuawa kikatili kwa wachimba migodi, bali kwa sababu ya nafasi mpya ya Kiswahili katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika.

Sarah Kimani alikuwa amesisimkia tangazo la Afrika Kusini kuwa itaanza kufundisha Kiswahili shuleni. Mwanzoni nilisita kidogo kukubali mahojiano.

Siku hizi nachelea mahojiano na vyombo vya habari. Nimehojiwa vya kutosha katika maisha yangu mafupi na ni bora kuwaachia magwiji au sijui wanaitwa magalacha halisi kutamalaki katika ulingo.

Hata hivyo, Sara alinirai sana hadi nikaraika. Nilifanya naye kazi zamani katika kampuni ya NMG wakati NTV ikiitwa Nation TV na kabla Nation FM kubadilishwa jina na kuwa Easy FM kisha tena Nation FM na kuachiwa kufa kifo cha mapema.

Sarah alifaulu kunipaka mafuta kwa mgongo wa chupa aliponiambia kwamba sijabadilika, miaka takriban 14 tangu nilipofanya kazi naye NMG.

Ukifika umri kama wangu unaanza kuhangaishwa na suala zima la umri. Mtu akikuhadaa kidogo kwamba hujazeeka unaweza kumfanyie lolote. Labda ndiyo maana niliraika kwa urahisi na Sarah, ingawa ukweli ni kwamba miguu yangu haishiki tena na uso umepiga mapeto na mwili kusinyaa. Ninajaribu kukinga jua kwa ungo, nitaweza?

Nilimwambia Sarah katika mahojiano yangu kuhusu furaha yangu kwa upanuzi wa Kiswahili barani Afrika kwa jumla na hasa Kusini mwa Afrika.

Afrika Kusini wanatambua Uafrika wao uliofichama katika Ubantu wa Kiswahili hata labda kuwashinda wakazi wenyewe wa Afrika Mashariki. Nchi ambayo ina lugha zake rasmi 11 kuamua kuongeza lugha nyingine ya nje katika zile zinazofundishwa shuleni ni tendo la ujasiri mkubwa. Yamkini watu wa Afrika Kusini ni miongoni mwa watu wanaothamini umuhimu wa lugha. Si ajabu kwamba hapo awali mwanasiasa Julius Malema alikuwa tayari amekifungamanisha Kiswahili na Uafrika mzima.

Baada ya kauli yangu ya pongezi kuhusu uamuzi wa serikali ya Afrika Kusini na urahisi wa kukijua Kiswahili, Sarah aliongeza lake katika taarifa yake iliyopeperushwa kote yanakofika matangazo ya SABC. Alisema Wakenya wanaotea nafasi za kwenda kufundisha Kiswahili Afrika Kusini.

Rafiki yangu Maulid Kambaya wa ITV alikuwa kanisukumia taarifa kwamba Watanzania wanaotea nafasi za ajira kwenda kufundisha Kiswahili Afrika Kusini.

Nikajiuliza mwenyewe, je, Watanzania wanajua kwamba Wakenya wanaotea nafasi za ajira za Kiswahili Afrika Kusini? Je, Wakenya wanajua kwamba Watanzania wanaotea nafasi za ajira za Kiswahili Afrika Kusini? Je, wote wanajua kwamba ni kawaida kuwa na kinyang’anyiro hiki kati ya Wakenya na Watanzania kwa nafasi za ajira za Kiswahili za nje ya nchi?

Watu wa Afrika Kusini wanataka kujiendeleza au kuwaundia nafasi za ajira Wakenya na Watanzania? Huu uzalendo wa Wakenya na Watanzania utatuua!

Prof. Ken Walibora ni msomi wa fasihi, mwanahabari na mwandishi mtajika katika ulimwengu wa Kiswahili