Diwani ya Sauti ya Dhiki ni tawasifu ya Abdilatif Abdalla

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, August 15  2018 at  07:50

Kwa Muhtasari

Mtunga blabu na mtunga utangulizi, hawana ujasiri alionao mshairi Abdilatif Abdalla kutufichulia bayana kwamba mashairi katika diwani ya Sauti ya Dhiki yameandikiwa gerezani, kwamba mashairi haya yanaingia katika utamaduni wa miaka na mikaka ya fasihi ya gerezani.

 

KINA CHA FIKIRA

NILIPATA fursa ya kuwasilisha makala juma lililopita katika kongomano la CHAKITA huko Eldoret kuhusu mshairi mkongwe Abdilatif Abdalla. Nataka leo nikupeni ijapo kwa kiduchu yale niliyokuwa nayo.

Kimsingi makala yangu ilijaribu kujibu swali; je, u wapi utawasifu wa Sauti ya Dhiki? Nami ninasema baada ya blabu na utangulizi kudokeza ufungamano kati ya diwani hii na maisha ya mtunzi, mtunzi mwenyewe ndiye anayetoboa waziwazi tena bila kusitasita kwamba mashairi haya yanazungukia maisha yake.

Mtunga blabu na mtunga utangulizi, hawana ujasiri alionao mtunzi kutufichulia bayana kwamba mashairi haya yameandikiwa gerezani, kwamba mashairi haya yanaingia katika utamaduni wa miaka na mikaka ya fasihi ya gerezani.

Mtunzi anafafanua kwamba mashairi yote isipokuwa “N’sharudi” alilolitunga baada ya kutoka jela, ameyaandika akiwa jela.

Alikuwa kafungwa tangu Machi 1969 hadi Machi 1972 kwa kosa la uchochezi. Kwa hiyo ni mtunzi mwenyewe katika dibaji ndiye anayejasiria kutueleza muktadha ambamo mashairi yameandikwa. Kisha anasema:

Mashairi yaliyomo humu yanahusiana na yaliyonifika hata ikabidi nifungwe; kifungo chenyewe; niliyokuwa nayo moyoni; imani yangu na maoni yangu kuhusu yaliyokuwa yakitendeka nje ya kuta za gereza. (xiii)

Tukichunguza kwa makini tunakuta kwamba Abdilatif Abdalla anaorodhesha mambo kadha wa kadha (1) muktadha na sababu ya kufungwa (“yaliyonifika hata ikabidi nifungwe”); (2) usimulizi kuhusu ufungwa wake (“kifungo chenyewe”); (3) hisia na fikra zake (“niliyokuwa nayo moyoni”) (4) itikadi na msimamo wake kuhusu nchi yake, bara lake na dunia yake (“imani yangu na maoni yangu kuhusu yaliyokuwa yakitendeka nje ya kuta za gereza”).

Ni nini hapa ambacho hakina mwelekeo wa kitawasifu? 

Tawasifu ni nini hasa isipokuwa usimulizi wa maisha ya mtu kuhusiana na matukio, mawazo, na itikadi zake? Hamna katika  muhtsari wake wa diwani kipengele ambacho hakifungamani na simulizi ya maisha yake. Ndio maana si kutapatapa wala kusema uzushi kusema kwamba kwa mujibu wa maelezo yaliyo wazi kabisa ya mtunzi kwenye dibaji, diwani ya Sauti ya Dhiki ni tawasifu yake na inaangazia hususan ufungwa wake.

Diwani hii haina utawasifu tu endapo tunang’ang’ania kwa uaminifu usiopindika na usiosaili mambo, tamko la Lejeune kwamba sharti tawasifu iwe imetungwa kwa lugha tutumbi.  Hata hivyo hata maelezo yake dibaji yaliyoandikwa kwa lugha tutumbi yenyewe yanatoa muhtsari kuhusu yaliyomo katika mashairi kwa upande mmoja na hali kadhalika taarifa za kitawasifu kumhusu mtunzi. Kwa maneno mengine, dibaji ya Abdilatif Abdalla ni aina ya tawasifu ya maisha yake.

Kwamba dibaji ni tawasifu lisionekana jambo la ajabu.

Sidonie Mith na Julia Watson wameainisha aina 52 za simulizi za maisha.  Kwa mfano wanaorodhesha shajara (diary na journal), tarekhe (chronicle), usuli (geneology), tafakuri (meditation), barua (letter), historia simulizi (oral history), memoir (memua), personal essay (insha ya binafsi), testimonio na poetic autobiography tawasifu ya kishairi.