Wanahabari mahiri wanaokitetea Kiswahili kwa uvumba na ubani

Imepakiwa Tuesday November 6 2018 | Na KEN WALIBORA

Kwa Muhtasari:

Zama zile redio ikisema basi ni hivyo.

ZAMANI za utoto wangu redio ilitawala. Redio ilikuwa mali ya umma. Ukiwa na redio, unasikiliza na wengine, sio peke yako. Na kama redio imesema kitu basi ni hivyo.

Redio ikisema mtu amefariki basi amefariki. Mpaka leo nakumbuka vipindi mahsusi vilivyorushwa hewani kuchangia ukuzaji wa Kiswahili.

Kuna kipindi cha lugha kilichokuwa kinarushwa na Redio Tanzania, Dar es Salaam. Wazee mikota wa lugha kama Hamisi Akida, Salim Kibao na Jumanne Mayoka walikuwa wakijadili masuala anuwai ya lugha.

Nilikuwa sipitwi na vipindi hivyo. Vilinifundisha mengi katika lugha ya Kiswahili.

Walikuwa wakishatamka wazee hao basi redio imesema, na redio ikisema basi ni kweli.

Nchini Kenya Sauti ya Kenya ilikuwa na wazee kama vile Abdalla Barua, Abdalla Mwasimba, Hassan Mwalimu Mbega, Jay Kitsao, Karega Mutahi na Mohamed Bakari.

Wazee hawa walijadili fani mbali mbali za lugha na kutufumbua macho kuhusu usahihi wa kusema na kuandika. Miaka ilipopita majina mapya nayo yakaingia katika jopo la mabingwa.

Wakaibuka magwiji kama Kyallo Wadi Wamitila, Kazungu Kadenge, John Habwe, Rayya Timammy na Said A. Mohamed na Mwenda Mbatiah ambao walichangia kunogesha kipindi na kutufundisha Kiswahili. Walipozungumza, redio ilikuwa imesema, na redio ikisema basi ni hivyo.

Nimekumbuka historia hii yote kwa sababu nimeona hivi karibuni kama redio inatawala bado ingawa inatawala sambamba na vyombo vingine vya ushawishi mkubwa kama vile runinga na mitandao ya intaneti. Ilikuwa furaha ilioje kuona redio na runinga zimeunganishwa katika kurusha mbashara kipindi cha Kamusi ya Changamka katika enzi ya QTV na QFM.  Munene Nyaga na Nuhu Zuberi Bakari waliwafundisha wengi Kiswahili katika kipindi hicho. Isitoshe, Redio Citizen nayo ilikuwa pia na kipindi cha Bahari ya lugha ambapo Ali Hassan Kauleni na Jilani Wambura walikuwa wakizamia lulu na wakiwafundisha wasikilizaji kuhusu maswala mbalimbali ya lugha. Katika kipindi hiki cha baada ya kutoweka kwa QTV na QFM, na kipindi cha Bahari ya Lugha angalao bado kuna majukwaa ya kukiendeleza Kiswahili.

Mathias Momanyi yupo mstari wa mbele katika kipindi chake cha kila Jumamosi katika Redio Taifa. Naye Ali Hassan Kauleni na wenzangu kama Mwalimu Abubakar Tsalwa na Mwalimu Titus Sakwa na guru Ustadh Wallah bin Wallah, wanaendelea kutupa nuru ya Kiswahili katika kipindi cha Nuru ya Lugha kwenye Redio Maisha.

Mabingwa wawili

Isitoshe, nilifurahi sana kuwaona mabingwa wawili wa QTV na QFM, Munene Nyaga na Nuhu Bakari wakitumia runinga nyingine kutetea na kufundisha lugha.  Hata TBC nao huku Tanzania wamejitahidi kurushwa runingani vipindi vya Kiswahili kila Jumamosi.

Ninafarijika kuona kwamba mambo yaliyotekelezwa na wazee wa zamani, hayakupotea wala kwenda arijojo. Kipo kizazi kingine cha wakeretwa kilichopokezwa mikoba na kinaendeleza ufundishaji na utetezi wa Kiswahili kwa kutumia vyombo vya habari.

Nasema heko kwenu mabingwa nyote kwa juhudi zenu.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"

Share Bookmark Print

Rating