HADITHI: Mwinyi mbu mbu mbu, aanika uchi gwarideni

Na SAMUEL SHIUNDU

Imepakiwa - Thursday, October 27  2016 at  11:14

Kwa Mukhtasari

WATU wengi walichukulia kuwa urafiki kati ya Pengo, Soo na Sindwele ulianzia shuleni Maka. Ndivyo alivyoamini hata Pengo mwenyewe.

 

Watatu hawa walisomea katika shule moja ya upili kule Sidindi. Soo na Sindwele walimjua Pengo lakini Pengo hakuwajua kwa kuwa Pengo alikuwa kiranja maarufu shuleni.

Pengo alikuwa kiranja wa litajia aliyejukumiwa kuandaa misa shuleni. Alikuwa mtoto wa misa na ilidhaniwa kuwa angekuja kuwa padri baadaye.

Enzi hizo, parokia ya Sidindi ilikuwa na padri mzungu aliyekuwa pia mwalimu wa vijana hawa. Mzungu huyu alikuwa na hamu kubwa ya kujifunza lugha za huko Sidindi ili akubalike kama mwenyeji.

Wakaaji wa Sidindi walilipuuza jina lake gumu na wakaamua kumwita muthungu hadi Jumapili moja baada ya misa alipoyatamka aliyoyatamka.

Alipotua Sidindi, mzungu aliwateua wanafunzi wa kidato cha kwanza ili wamfunze lugha na miongoni mwao walikuwa Soo na Sindwele.

Akawauliza wamfunze salamu. Wakamfunza. Akafanya mazoezi hadi alipokuwa na uhakika kuwa anaweza kutamka yale aliyofunzwa na vijana.

Ilikuwa Jumapili moja baada ya misa alipoamua kujaribisha. “Mmeosha makalio yenu?” padri aliwauliza kwa furaha akitarajia kuitikiwa.

Badala yake, kauli ya padre ilipokewa kwa manung’uniko. Alikuwa anawatukana. Padri alirejelea salamu yake kwa sauti imara.

Wazee wa kanisa wakamwendea altarini. Wakamnong’onezea. Akaufyata. Tangu hapo akapata jina jipya, Makalio.

Padri akapoteza imani na wanafunzi, akamfuta Pengo kazi. Soo na Sindwele wakamhurumia Pengo Wakaamua kuwa wangekuwa rafiki zake.

Walipokutana shuleni Maka, hapakuwa na mjadala, walimfanya rafiki papo hapo. Soo na Sindwele waliukumbuka utundu huu.

Walimnunulia Wamatangi pombe na kumwambia kuwa Mwinyi alikuwa kaenda kusuluhisha migogoro ya mashamba. Sindwele akiwa mwalimu wa fasihi ya Kiswahili alikuwa amewafafanulia wenzake kuhusu kisa cha Nasaba Bora na migogoro ya mashamba.

Wakakipenda na kuwafafanulia wengine ambao hawakuwa wameisoma riwaya hiyo. Walimu wote isipokuwa Mwinyi, Mugabe na Wamatangi walijua. Dina na Harieta hawakujua kuwa walilakabiwa Lowela.

Mwinyi na rafiki zake walidhani malowela ni kisawe cha wakulima. Dina na Harieta walichukulia kuwa malowela ni mahawara. Kila mmoja alimwona mwenzake kuwa hawara.

Wanafunzi waliupokea ujumbe wa naibu mwalimu mkuu kwa mshangao. Walishangaa zaidi Mwinyi alipokiri kuwa alikuwa kaenda kusuluhisha migogoro ya mashamba.

Akiwa mwalimu wa Kiswahili, wanafunzi walimtarajia Mwinyi kujua maana ya kusuluhisha migogoro ya mashamba. Lakini Mwinyi hakujua maana, yeye alifundisha tu ufahamu kwa kisingizio cha kuwa na majukumu mengi.