http://www.swahilihub.com/image/view/-/1371404/medRes/344299/-/irlsspz/-/DNTURKANA2306v.jpg

 

Wajue Wasekuye

Vijana wa Gabbra

Picha/MAKTABA Vijana wa jamii ya Gabbra wakiimba wimbo wa vita katika tamasha za kila mwaka za utamaduni za Loiyangalani, Turkana. Wasekuye wanakaribiana sana na Wagabbra. 

Na MAKAVAZI YA TAIFA LEO

Imepakiwa - Thursday, March 22  2012 at  15:53

Kwa Muhtasari

Wasakuye hukaribiana sana na makabila ya Gabbra, Borana, na Merille. Walitengana wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kwani wengi wao walitorokea nyikani ili waepukane na serikali ya mkoloni iliyowataka waende wapigane nchini Burma barani Asia.

 

WASEKUYE wanapatikana katika mkoa wa Kaskazini Mashariki wilayani Moyale kwenye miji ya Wajir na Moyale. Wengine pia hupatikana katika viunga vya mji na barabara ya Dabell na Buna Wajir.

Wasakuye ni ndugu zao makabila ya Gabbra, Borana, na Merille. Walitengana wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kwani wengi wao walitorokea nyikani ili waepukane na serikali ya mkoloni iliyowataka waende wapigane nchini Burma barani Asia.

Wengi wa Wasakuye walioana na Wameerille, Waborana na Wagabbra na mila na tamaduni yao ilianza kudidimia kutokana na kukaa na hawa ndugu zao.

Sehemu wanayoishi Wasakuye ni kavu na haiwezi kustahimili kilimo hata kidogo hivyo basi Wasakuye huishi maisha ya kuhamahama angalau watafutie mifugo yao malisho tosha na maji masali ya kupikia na kunywa.

Hesabu ya Wasakuye kwa hivi sasa inafikia watu 10,123 wote wakikalia maeneo ya kaskazini mwa mji wa Wajir na Marsabit kwa upande wa kusini.

 

Hufanana na Wagabbra

Mila, tamaduni na itikadi za Wasakuye kufanana na zile za Wagabbra kwa vyovyote. Kilugha, Wasakuye huongea lugha za Kisomali na Kiswahili.

Wanapenda kufuga mifugo kama mbuzi, ngamia na kondoo kwani hao ndio wanaweza kustahimili hali ngumu ya ukame huko mkoani Kaskazini Mashariki.

Licha ya haya, Wasakuye bado ni jamii iliyobahatika sana kama mwana aliyezaliwa Ijumaa kwani mifugo wanaowafuga wamewahi kuzaana sana mpaka huwa wanawaleta baadhi ya masoko ya mifugo humu nchini ili kuwauza angalau wapate riziki na kitoweo, kweli Mungu sio athumani.

Vyumba wanamoishi ndani vimepambwa na vitambaa, vilivyoundwa na nyuzi ya makonge na kushikwa na ngozi nyororo kama kamba.

Juu ya paa, kumewekwa ngozi na udongo usioweza kuvuja hata kidogo wakati wa mvua, pia isitoshe, kuna nyufa zilizoachwa ili kuleta hewa safi ya kuvutia na kukata na shoka. 

Wanawake toka kabila la Wasakuye hutakiwa kusuka nywele saa zote kama ishara ya heshima kwa wanaume na wakongwe, nywele hushikwa pamoja na aina ya ngozi kilichopakwa rangi aina ya kijivu au ngeu nyekundu. Wasichana nao huwa wanastahili kutunza nywele sawa na akina mama.

Wanaabudu Mungu mmoja

Wengi ni waumini wa dini ya Kiislamu, na wanaamini Mungu wao mmoja tu. Kallu au Qallu, anayetegemewa kwa saa zote na pia kuna aina ya vikundi maalum vya kiumri vinavyoitwa Gada huku vikiwa na vitengo pia vya kiukoo kama kenda zote zikiitwa Migo.

Jamaa hawa hutenga wasichana na wavulana wakati wa kuwapasha tohara, wakati huu, vijana huitarajiwa kuvaa ngozi mwili na kofia iliyotengenezwa kuwakinga ikiwa wamevamiwa na adui.

Mnamo miaka ya 1965-1968, Wasakuye walikuwa na wakati ngumu kutokana na uvamizi wa wale wanaojulikana kama Mashifta na wengi wao walifiwa na jamaa kutokana na kupigana na Mashifta ili kulinda mipaka yao. Fauka ya hayo, Wasakuye bado wamesimama imara kusudi walinde mipaka yao ili wasivamiwe.

Jamii hii hata hivyo imo hatarini ya kumezwa na jamii ya Wasomali.