http://www.swahilihub.com/image/view/-/1525824/medRes/390455/-/rxpv9oz/-/Shikuku.jpg

 

Tofauti kati ya Marama na Abawanga

Martin Shikuku

Mwanasiasa Martin Shikuku. Picha/MAKTABA 

Na SWAHILI HUB

Imepakiwa - Friday, October 5  2012 at  14:19

Kwa Muhtasari

Wabawanga sawa na Wabantu wengine walitoka Cameroon. Walipofika mlima Elgon walikumbana na Wasebeyi na Wasabaot ambao hawakuwaruhusu kutulia huko na ndiposa wakaamua kuhamia Mumias - wakiufuata Mto wa Lusimu. Waliunganishwa na mfalme Mumias Wanga. Ni tofauti na Wamarama, Wabanyala na Wamarachi ingawa lafudhi zao zinakaribiana.

 

KABILA la Abawanga hupatikana Wilayani Butere Mumias katika Mkoa wa Magharibi. Watu wengi wamekuwa na shida ya kuwatofautisha Wamarama, Wabanyala, Wamarachi na Abawawanga kwani lafudhi zao zinafanana sana.

Historia fupi kuhusu kabila hili ni kwamba asili yao ni huko Cameroon. Kutokana na mrundikano wa watu, Wabawanga waliamua kutafuta makao kwingineko.

Hatua kwa hatua waliweza kusafiri hadi mlima Elgon kupitia nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (awali ikijulikana kama Zaire). Wasebeyi na Wasabaot waliomiliki ardhi ya mlima huo hawakuwaruhusu kutulia huko na ndiposa wakaamua kuhamia Mumias - wakiufuata Mto wa Lusimu.

Kufika Mumias walikabiliwa na shida mbalimbali zikiwemo kuvamiwa na jirani zao Waluo. Ni wakati huu ndipo kiongozi shupavu wa enzi za wakoloni, mfalme Mumia Wanga alibuka na kuwaunganisha pamoja na watu wake ndipo wakaweza kuwashinda Wajaluo. Ushupavu na ujasiri wa Mumia ulikithiri mipaka na akaweza kujizolea sifa kote nchini na barani Afrika.

Kuhusu mila na utamaduni wa watu wa kabila hili ni kwamba mvulana hupaswa kutahiriwa punde tu atimizapo umri wa kati ya miaka 10 - 15. Ili kudhihirisha 'uanaume' kijana huhitajika kukabiliana na 'Kisumu' nyumbani kwao mbele ya kadamnasi ya watu.Mvulana atimizapo umri wa zaidi ya miaka 18 na awe anataka kuoa, huomba idhini ya wazazi au wajomba zake.

Iwapo watakubali, majadiliano juu ya mahari hufanywa na pande zote mbili (ukoo wa mvulana na msichana).Mara nyingi mifugo kama vile ng'ombe au kondoo ndio hulipwa kama mahari.

Kumlea mwana

Kiasi cha mahari hutegemea kiwango cha elimu aliyopata msichana. Punde tu baada ya mtoto kuzaliwa ni nyanya yake ndiye anayestahili kuwa mtu wa kwanza kumlea na wakati huo huo kumpa jina.

Jina la ukoo hupewa kulingana na wakati au sehemu aliyozaliwa. Kwa mfano, mtoto azaliwaye barabarani huitwa Nanjira na yule wa wakati wa mavuno huitwa Nechesa.Kuhusu dini, idadi kubwa, karibu asilimia 60 ni Waislamu huku wengine wakiwa Wakristu.

Bila ya kupaka mafuta mgongo wa chupa, kabila hili lina mengi ya kujivunia. Kwa upande wa sekta ya kilimo Abawanga wamepiga hatua si haba kwani ni katika sehemu yao ndiko kunakuzwa miwa, mahindi na mihogo.

Pia, katika kabila hili. kumezaliwa na kulelewa mashujaa mbalimbali wakiwemo wa kisiasa kama vile aliyekuwa wakati mmoja Katibu Mkuu wa Ford-Kenya, Bw Martin Shikuku, mbunge kwa muda mrefu, Bw Ellon Wameo na Waziri msaidizi, Bw Wycliffe Osundwa.