http://www.swahilihub.com/image/view/-/1529114/medRes/408227/-/st1cjnz/-/Luhyaa.jpg

 

Kabila kubwa la Abaluhya

Musalia Mudavadi

Mgombea Urais, Musalia Mudavadi wakati wa mahojiano na Sunday Nation, Oktoba 2012. Picha/DENNIS OKEYO 

Na SWAHILI HUB

Imepakiwa - Tuesday, October 9  2012 at  15:26

Kwa Muhtasari

Asili ya Wamaragoli ni Uganda. Katika Kenya Wamaragoli wanapatikna katika Wilaya za Vihiga na Kakamega.

 

Kabila la Wamaragoli ama "Abalogoli" ndilo kabila kubwa katika jamii ya Waluhya. Kabila hili linapatikana katika Wilaya za Vihiga na Kakamega, mkoani Magharibi.

Hata hivyo, baadhi yao wamesambaa katika sehemu nyingine kama vile Wilaya za Bungoma na Trans Nzoia kwa minajili ya kilimo na biashara.

Historia yadhihirisha kwamba asili ya Wamaragoli ni Uganda. Jina Maragoli lilitokana na mwanzilishi wa kabila hili aliyefahamika kama Mlogoli. Mkewe Mlogoli alifahamika kama Kadesa.

Kwa ari ya maji masafi na udongo wenye rutuba, Mlogoli na mkewe walisafiri kutoka Uganda hadi sehemu za Busali na Sabatia nchini Kenya. Hii ilikuwa ni miaka ya zamani hata kabla ya kuwasili kwa wabeberu nchini.

Katika eneo la Sabatia, Mlogoli na mkewe walitulia na kujaliwa kupata watoto tisa. Baada ya watoto hao kukua na kuoa kutoka kwa jamii zilizowazingira, mbari au koo 9 zilizaliwa.

Baadhi ya koo hizo ni Avamari, Valogoro na Vavamari-Vagonda. Watu wa koo hizi wanapatikana Maragoli ya Kati na Kusini. Kwa maana ni wa damu moja, watu hawa hawaruhusiwi kuoana. Wakitaka kuoa ni lazima wajipatie wachumba kutoka kwa koo zinazopatikana Rugali na Maragoli ya Magharibi, kama vile Abamasingila, Abasali na Abasalia.

Kuhusu tamaduni za Wamaragoli ni kwamba nyanya yake mtoto ndiye humpa jina punde tu azaliwapo. Jina la mababu waliokufa ndilo hupewa mtoto kama njia mojawapo ya kuwakumbuka na kuwaheshimu waliokufa. Pia sehemu na wakati azaliwapo mtoto azaliwaye njiani huitwa chukunzira.

Mila ya Wamaragoli haimruhusu mvulana kutotahiriwa. Mvulana hupashwa tohara akiwa na umri wa miaka minne na isiyozidi 10. Kikundi cha vijana kinachotaka kupashwa toftara hupelekwa mtoni alfajiri na kutahiriwa baada ya kuoga. Baadaye hupelekwa katika nytunba yao rasmi ambayo hufahamika karna mdumi.

Kijana haruhusiwi kuingia nyumba nyingine hadi pale atakapopona na kuombewa, na wakati huo huo kupewa wosia wa wazee. Ni wakati huu ndipo kijana hukitupilia mbali kila kitu cha zamani na kupewa vitu vipya kama vile mavazi na malazi. Hii huwa ni ishara kwamba ameepuka mambo ya kitoto na sasa ni "mwanaume."

Upande wa ndoa, ni mvulana ndiye humtafuta mchumba na baada ya kumpata aliyempendeza, huwafahamisha wazazi wake na majadiliano juu ya mahari hufanywa na pande zote mbili (ukoo wa msichana na wa mvulana).

Awali, mifugo na nafaka ndizo zilipeanwa kama mahari. Siku hizi watu wengi hutumia pesa badala ya mifugo.

Baadhi ya mimea wanayokuza ni mahindi, mawele, mtama na maharagwe. Mifugo wao ni kama ng'ombe, kuku, kondoo na mbuzi.

Katika upande wa maendeleo, Wamaragoli wamepiga hatua si haba; lakini kulingana na wazee waliohojiwa na mwandishi wa Taifa Leo wanatazamia mengi.

Walifichua kwamba milango ya maendeleo ilifunguliwa na mwakilishi wao Bungeni na aliyetokea kuwa mtu wa kutajika katika baraza la mawaziri wakati huo, marehemu Moses Mudavadi. Marehemu alikuwa baba yake Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Bw Musalia Mudavadi.

Kwa upande wa biashara, kabila hili limeweza kuwakuza wafanya biashara wa kutajika kama vile Bw lbrahimu Ambwere ambaye mchango wake kwa jamii yake na taifa nzima kwa ujumla ni mkubwa mno.