Mke mwenye busara

Na SIZARINA HAMISI

Imepakiwa - Monday, June 11  2018 at  09:06

Kwa Muhtasari

Mwanamke mwenye busara anaelewa wajibu kama; wajibu kama mama iwapo umejaliwa watoto na mipaka ya ndugu, jamaa na marafiki.

 

MKE mwenye busara huelewa mipaka.

Mipaka hii inahusu wajibu kama mke, wajibu kama mama iwapo umejaliwa watoto na mipaka ya ndugu, jamaa na marafiki.

Mipaka ya mke katika uhusiano na mumewe inahusu zaidi wajibu wake katika ndoa. Kwani wapo akina dada walio wavivu kupindukia, mwanamke kama huyu anathubutu kuuchapa usingizi na kumuachia majukumu yote msichana wa kazi.

Mumewe anapoamka kwenda kazini ama kwenye majukumu yake yeye atabaki amelala baada ya kumuagiza msichana wa kazi apike chai na atayarishe nguo za mumewe. Kwamba hata mumewe anapoondoka asubuhi, yeye hana habari amevaa nguo gani, hajui amependeza au haikumpendeza.

Ataendelea kuuchapa usingizi na akiamka saa nne asubuhi, chumba kichafu na jambo la kwanza ni kuchukua simu na kuingia kwenye mtandao kuangalia umbea wa siku hiyo; na bado unajiita mke dadangu?

Kuongeza chumvi kwenye kidonda, unakuta dada huyu anazaa watoto kama kuku wa kienyeji.

Hajali wala kuangalia hali halisi na maisha yaliyopo nyumbani kwake na huenda maisha yao ni ya kuhangaika lakini hachukui hatua ya kuhakikisha watoto wanapatikana kwa mpangilio.

Unakutana na mwanamke ana watoto saba lakini wanaishi chumba kimoja.

Nalisema hili baada ya kushuhudia dada mmoja akisumbuka na watoto wanne ambao wamepishana kwa miezi na si mwaka. Nami kama kawaida huwa napenda kudodosa. Nikamwuliza sababu ya kuzaa watoto kama mayai ya chura. Alichoniambia nilichoka, nikaamini kama ataendelea vile basi atajaza timu ya mpira na wachezaji wa akiba.

Alinieleza kuwa mumewe ni askari na kuna kipindi kutokana na kazi yake, huwa anarudi nyumbani muda usio maalum.

Yeye akaamini mumewe ana mwanamke wa nje, kwa vile haki yake ya ndoa kuipata imekuwa patashika.

Kwa hiyo siku akipatikana kutoa huduma kwa mkewe, yeye huwa hajali wala kuangalia iwapo siku hiyo anaweza kushika mimba, anamkaba mumewe hadi apate haki yake.

Njia nyingine

Hii tabia ikasababisha kila akikutana na mumewe anaruka na ujauzito kitu ambacho hakimpi taabu kwa vile anaamini hana njia nyingine ya kupata haki yake kwa mumewe.

Kwa upande mwingine iwapo kaka nawe uko kwenye ndoa, shiriki kwenye kupanga idadi ya watoto mnaoweza kuwamudu. Hakuna ufahari wowote kumzalisha mkeo kama kuku wa kienyeji.

Halikadhalika, mkeo hukumuoa kumuweka mapambo nyumbani kwako. Anahitaji huduma muhimu kutoka kwako hivyo usimnyime ama kumuwekea udhibiti wa hiyo huduma.

Unamnyima haki yake, akaipate wapi au unataka kumlazimisha achepuke nje ya ndoa ili upate sababu ya kumtelekezea mtoto?

Hivyo dada, nazungumzia mipaka kama mke. Elewa nafasi yako katika kuleta maendeleo na ufanisi katika ndoa yako.

Jambo unalotakiwa kutambua ni kuwa tupo wanawake wengi na wengi tena wazuri, na wanaokua kujipamba ili kuwanasa waume za watu.

Kwa vile ndani ya nyumba havipati, sababu umeshindwa kuweka mikakati na mipaka, sio ajabu akili ya mumeo ikahamia nyumba ndogo. Na nyumba ndogo huwa wanajua kutumia fursa.

Mwanamume akionja, atachonga mzinga na kumsahau mkewe. Akina kaka hebu muwe na utu. Mpende mkeo. Huyo anayekuzuzua anakupenda kwa vile una kitu ukiishiwa humuoni.

Hebu heshimu ndoa kwa kumjali mkeo sio kumzalisha mfululizo au kumpatia haki ya ndoa kwa mgao au kutochukua hatua ya kujadiliana naye kuhusu umuhimu wa kupanga idadi ya watoto ambao mnaweza kuwatunza na kuwalea bila changamoto nyingi.

Natumaini nimeeleweka.

 

 

Mke alikataa kuja nyumbani nikaoa mwingine

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Tuesday, February 20  2018 at  08:45

Kwa Muhtasari

Mke wangu alipata kazi mbali na nyumbani na anaishi huko; ni siku nyingi hajaja nyumbani na nikimuuliza anadai hana pesa; nishauri.

 

SHANGAZI AKUJIBU

Mke alikataa kuja nyumbani nikaoa mwingine

NINA mke na watoto watatu. Mke wangu alipata kazi mbali na nyumbani na anaishi huko. Ni siku nyingi hajaja nyumbani na nikimuuliza anadai hana pesa. Nimeshindwa kuvumilia na nimepata mwanamke mwingine ambaye sasa ninaishi naye na pia ana mimba yangu. Mke wangu alijua na akanipigia simu akitishia kuwa akimpata mwanamke huyo nyumbani kwetu atakiona. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nitakulaumu kwa kukimbilia kuoa mwanamke mwingine eti kwa sababu mke wako amekawia kuja nyumbani. Kabla hujachukua hatua hiyo ungejitolea mwenyewe kumtembelea huko anakofanya kazi ili ujue shida iliyopo kwani wewe ndiye mume wako. Itabidi umwambie ukweli mwanamke huyo kwamba mke wako hamtaki hapo ili aondoke kwani hujui amepanga kuchukua hatua gani.
   

Nashuku anidanganya

HUJAMBO shangazi? Mimi nahisi kuwa mwanamume mpenzi wangu ananidanganya. Sababu ni kuwa bado anaweka nambari ya simu ya mpenzi waliyeachana. Nashangaa ni kwa nini bado anaweka namba hiyo kama kweli waliachana. Nishauri.

Kupitia SMS

Huenda mpenzi wako aliamua kuwa wataendelea kuwa marafiki na huyo wake wa zamani hata baada ya kuachana. Kama una wasiwasi kuhusu yeye kuendelea kuwa na nambari hiyo, ni vyema ushauriane naye kuhusu jambo hilo badala ya kulinyamazia.

Nimetemwa

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 20 na nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa. Sasa amenigeuka ghafla ananiambia eti hanitaki nitafute mwingine. Nampenda sana na sijui nitafanya nini. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni muhimu ufahamu kuwa hakuna mikataba inayowekwa kudumisha uhusiano kwa hivyo mmoja wa wahusika akihisi kujiondoa kwa sababu moja au nyingine ana haki ya kufanya hivyo. Kama mwenzako amekwambia hakutaki, huna la kufanya ila kukubali uamuzi wake kwa sabu huwezi kumlazimisha akupende.

Amesema hataki kuoa
HUJAMBO shangazi? Nimekuwa na uhusiano na mwanaume fulani kwa miaka sita sasa na amekuwa akila pesa zangu tu. Sasa amenipa mimba na ananiambia hayuko tayari kuoa. Yeye anaishi Nairobi nami naishi Mombasa. Je, atanioa au la?

Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini amekuwa akila pesa zako ilhali yeye ndiye mwanaume anayefaa kukupa pesa za kugharamia mahitaji yako. Pili, sielewi ilikuwaje ukakubali kupata mimba yake bila hakikisho kutoka kwake kwamba atakuoa. Madai yake kuwa hayuko tayari ni dalili za kutaka kujitenga nawe na usishangae akikutema. Ushauri wangu ni kuwa uwe tayari kwa chochote kile kutoka kwake.

Nimembania asali

SHANGAZI nina mpenzi tunayependana sana na tumekuwa pamoja kwa mwaka mmoja sasa. Ameahidi kunioa na amekuwa akiniomba mahaba lakini naogopa kwani sijawahi kufanya hayo maishani mwangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Jambo analotaka mwenzako litategemea hiari yako wala si lazima. Hasa, tendo la ndoa linafaa kusubiri hadi watu wanapooana ingawa baadhi ya watu hukubaliana kuanza mapema. Kama unahisi huwezi kwa sasa, mwambie mwenzako na umuelezee sababu. Kama kweli anakupenda ataelewa.

Nimeambiwa anafuatafuata vidosho

MPENZI wangu alinipa mimba punde tu nilipomaliza shule ya msingi na bado tuko pamoja. Wazazi wangu wamenipeleka kusomea ualimu na sasa nimesikia fununu kuwa huyo mpenzi wangu ameshikana na wasichana wengine. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Unasema umepata fununu tu kuhusu huyo mpenzi wako wala huna hakika. Tafuta jinsi ya kuthibitisha fununu hizo ili ujue ukweli. Ukipata ni ya kweli, haina haja ya kuendelea na uhusiano na mtu ambaye si mwaminifu kwako.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Mke wangu ametoroka na rafiki yangu wa mtaani

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Tuesday, February 6  2018 at  12:50

Kwa Muhtasari

Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili alihama ghafla mtaani bila kuniambia na mwanamume rafiki yangu pia amehama na nimechunguza nikagundua wameenda kuishi pamoja; nifanyeje?

 

SHANGAZI AKUJIBU

Mke wangu ametoroka na rafiki yangu wa mtaani

HUJAMBO shangazi? Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili alihama ghafla mtaani bila kuniambia. Mwanamume rafiki yangu pia amehama na nimechunguza nikagundua wameenda kuishi pamoja. Sikujua kuwa wamekuwa na uhusiano hata mwanamke huyo ana mimba ya mwanaume huyo! Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, ni wazi kuwa mwanamke huyo amekuwa akikudanganya kuwa ni wako huku akimgawia asali rafiki yako. Hatua yake ya kushikana na rafiki yako huyo na kupata mimba yake ni ishara kamili kuwa amemchagua yeye na hana haja nawe. Huo ni uamuzi wake na huwezi kumlazimisha akurudie. Kubali na uendelee na maisha yako.

Alinihadaa nikaenda shamba, sasa ameoa

HUJAMBO shangazi? Nimeolewa na ninampenda sana mume wangu. Mwaka uliopita alinidanganya niende kwetu na mtoto wetu na akaahidi kuja kunichukua. Lakini baada ya wiki mbili alinipigia simu akaniambia ameoa mke mwingine. Sijarudi kwake na pia ameacha kugharamia mahitaji ya mtoto. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni wazi kwamba mume wako aliamua kuchukua njia ya mkato kukutaliki. Ni jambo ambalo amekuwa akipanga na hatimaye amefaulu kwa sababu sasa uko kwa wazazi wako naye ameoa mke mwingine. Ingawa amekuacha, unaweza kumpeleka kortini ili alazimishwe kugharamia malezi ya mtoto wenu.

Aliniambia hajaoa ila tetesi zasema kaoa

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 21 na kuna mwanaume tunayependana sana. Tulipokutana mara ya kwanza nilimuuliza iwapo ameoa akaniambia hajaoa. Hata hivyo, hivi majuzi mtu fulani aliniambia ameoa na nilipomuuliza tena akakana kabisa. Sasa nimechanganyikiwa, sijui ni nani anayesema ukweli. Nishauri.

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, mpenzi wako amekwambia mara mbili sasa kuwa hajaoa na unafaa kumwamini hadi utakapothibitisha habari za aliyekwambia kuwa ameoa. Jinsi pekee ya kujua ukweli ni kwenda kwao nyumbani na kuwauliza jamaa zake. Ikiwezekana, fanya hivyo.

Baada ya kunitusi eti nina sura mbaya, ananiomba msamaha

SHIKAMOO shangazi! Mwanaume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili tuligombana majuzi na akanitusi akisema mimi ni sura mbaya hata hajui amekuwa akitafuta nini kwangu. Nilimpenda kwa moyo wangu wote na matamshi yake hayo yaliniuma sana moyoni na nikajiambia kuwa sitawahi kuongea naye tena maishani. Siku mbili baadaye nilishangaa aliponipigia simu kuomba msamaha eti matamshi yake yalitokana na hasira. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mtu anaweza kusema chochote anapokuwa na hasira. Kama mwenyewe ndiye aliyeomba uhusiano huo na kuungama kuwa anakupenda haiwezekani kwamba umegeuka kuwa sura mbaya baada yenu kukosana. Isitoshe, amekuomba msamaha na kukwambia hayo yalitokana na hasira. Jaribu kumuelewa.

Ninapenda burudani hadi siridhiki hata na mume mmoja

HUJAMBO shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28 na sina mpenzi kwa sasa. Sababu ya kukosa mpenzi ni kuwa ninapenda sana burudani na kila ninapokuwa na uhusiano huwa siridhiki inabidi nitafute pembeni na nikigunduliwa ninatemwa. Je, nina kasoro?

Kupitia SMS

Siwezi kuita tabia yako hiyo kasoro kwa sababu watu wameumbwa kwa namna tofauti na labda hayo ndiyo maumbile yako. Hata hivyo ni tabia mbaya kuweka mbele mambo hayo katika uhusiano. Kuna tofauti kubwa kati ya mapenzi ya dhati na tamaa.

Mume mpenzi wangu haamini ni yeye tu

HUJAMBO shangazi? Nina mpenzi ninayempenda kwa dhati. Ninaishi mbali naye na amekuwa akinishuku kuwa nina wanaume wengine. Nimemhakikishia kuwa ni yeye tu lakini hataki kuniamini. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sijui mwenzako anataka umwambie nini tena kama umemhakikishia huna mwingine ni yeye tu na hataki kuelewa. Mwambie kama hakuamini ahamie unakoishi ili thibitishe mwenyewe.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Mke tuliyeachana amenitenganisha na watoto

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Wednesday, January 31  2018 at  10:38

Kwa Muhtasari

Tuliachana na sasa amenikataza kuwaona au kuwasiliana na watoto tuliozaa pamoja; nifanyeje?

 

SHANGAZI AKUJIBU

Mke tuliyeachana amenitenganisha na watoto

KWAKO shangazi. Nilikuwa nimeoa lakini mke wangu akaniacha kwa sababu ya fitina za majirani. Alirudi kwao na huko akaolewa na mwanaume mwingine. Hata hivyo, waliachana majuzi sasa yuko kwao. Tatizo ni kuwa amenikataza kuwaona au kuwasiliana na watoto tuliozaa pamoja. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama ameachana na mwanamume aliyemuoa na sasa yuko kwao, hana sababu ya kukuzuia kuwaona au kuwasiliana na watoto wenu kwa sababu hiyo ni haki yako. Ushauri wangu ni kuwa utumie utaratibu wa kisheria kupitia mahakamani ili upate rasmi ruhusa ya kuwaona watoto wako.

Hataki kuniambia SMS ni za nani

NINA umri wa miaka 27 na mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu. Nina mpenzi ninayempenda sana. Hata hivyo, nimekuwa nikiona SMS za kimapenzi katika simu yake kutoka kwa mwanamke mwingine na nikimuuliza haniambii chochote cha maana. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Maelezo yako yana maana kwamba mwenzako ana mpenzi mwingine wa pembeni lakini hajakubali wala kukataa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba ana mwingine na ndiyo maana anakosa cha kukuambia kwani anajua akikuambia ukweli utakasirika na kumuacha. Badala ya kuendelea kuwa gizani, ni heri ujiondoe katika uhusiano huu.

Nilimtoa mbali sana, sasa amenitema

HUJAMBO shangazi? Kuna mwanaume tuliyependana miaka miwili iliyopita akiwa bado chuo kikuu ingawa mimi ninafanya kazi. Nimekuwa nikimsaidia kwa mahitaji yake ya kifedha hadi akamaliza masomo na akapata kazi. Ajabu ni kuwa punde tu baada ya kupata kazi aliniacha akashikana na mwanamke mwingine. Ninajuta sana kwa muda na pesa zangu ambazo nilitumia kwa ajili yake. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba mwanamume uliyemsaidia alipokuwa na haja ameamua kulipa hisani yako kwa kukutema kimadharau kwa sababu ya mwanamke mwingine. Ushauri wangu ni kwamba usijute. Badala yake, jaribu juu chini umsahau, utapata mwingine.

Anitafuta na tayari nishapata mwingine

SALAMU shangazi. Mpenzi wangu niliyekuwa nimempa moyo wangu wote alikatiza mawasiliano ghafla bila sababu na akabadilisha namba yake ya simu. Nafikiri alipata mwingine na hakutaka kuniambia ukweli. Mwezi uliopita nilishtuka aliponipigia simu baada ya miaka mitatu akidai eti bado ananipenda ilhali nimeshapata mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea ni nani unayempenda zaidi kati yake na uliye naye sasa. Kama utamchagua yeye, hakikisha amekupa sababu za kutosha za kutoweka na kupuuza simu zako kwa miaka yote hiyo. Labda unavyosema ni kweli kwamba alikuwa amepata mwingine na huenda wamekosana na ndiyo maana ameamua kurudi kwako.

Asali ya pembeni imenitia kichaa

NIMEOLEWA kwa miaka miwili na nina mtoto mmoja. Hata hivyo nimeshindwa kumuacha mpenzi wangu wa awali na tumekuwa tukikutana na kufanya mambo yetu pembeni. Ninajua kwamba mume wangu akigundua nitakuwa mashakani lakini mahaba ninayopata kutoka kwa mwanaume huyo siwezi kuyapata kwingine na sidhani ninaweza kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini ulimuacha mpenzi wako wa awali kama kweli ndiye anayekupa mahaba unayostahili. Pili, ni vyema kwamba unacheza na moto ukijua unaweza kukuchoma. Utajua kuwa huo ni mchezo hatari pale mume wako atakapojua kuhusu vituko vyako ama utakapopimwa uambiwe una Ukimwi. Shauri yako!

Nitaacha masomo ili niolewe?

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 22 na ninasomea udaktari katika chuo kikuu. Mpenzi wangu ni daktari na tayari anafanya kazi. Sasa anataka tuoane lakini mimi naogopa kwani bado ninasoma. Nimeshindwa kuamua na ndiyo sababu nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni vyema kuwa unatambua umuhimu wa masomo yako yakilinganishwa na uhusiano wa kimapenzi. Ninaamini hofu yako ni kuwa ndoa itaathiri kwa kiwango fulani umakinifu wako katika masomo. Hiyo ni kweli. Ushauri wangu ni kuwa umwelezee mpenzi wako wasiwasi wako na umsihi akupe muda umalize masomo ndipo muanze maisha pamoja. Kama anakupenda atakubali. Akikataa, itabidi uamue lililo muhimu kwako kati ya masomo na ndoa kisha ukate kauli.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Mtoto amekataa kabisa kutoka chumbani mwetu

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Tuesday, January 23  2018 at  07:50

Kwa Muhtasari

Tabia ya mtoto inatunyima raha zetu chumbani ingawa mama yake haonekani kujali; nifanye nini?

 

SHANGAZI AKUJIBU

Mtoto amekataa kabisa kutoka chumbani mwetu

HUJAMBO shangazi? Nimeoa na mtoto wetu wa kwanza ni msichana ambaye sasa ana umri wa miaka mitano. Tatizo ni kuwa amekataa kabisa kutoka katika chumba chetu cha kulala ingawa ana chumba chake. Tabia yake hiyo inatunyima raha zetu chumbani ingawa mama yake haonekani kujali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ingawa bado ni mtoto, binti yenu, katika umri wake huo, hafai kuwa akilala katika chumba chenu. Wewe na mke wako mna wajibu wa kumfunza kulala katika chumba chake. Kulingana na maelezo yako, ni kama kwamba mke wako hajaathiriwa na jambo hilo. Ni vyema uketi chini naye mlizungumzie na kupata suluhisho.

Najaribu kurekebisha mienendo ya mke wangu ila hanielewi

SHANGAZI mimi nimeoa na nimeishi na mke wangu kwa miaka miwili sasa. Lakini naona ameanza vinjia vingi na nikijaribu kumrekebisha hanielewi kabisa. Nampenda sana na sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Sielewi unamaanisha nini ukisema mke wako ameanza vinjia vingi. Kama ni tabia ambazo unahisi zinaweza kuathiri vibaya ndoa yenu, basi mwelezee wazi awache ili kulinda ndoa yenu. Akishindwa kujirekebisha utaamua iwapo utaendelea kumvumilia ama mtakubaliana kuachana.

Nimechoshwa na tabia ya wazazi wa mke kuniomba pesa

SALAAM aleikum shangazi. Mimi nina mke na tumejaliwa mtoto mmoja. Tatizo ni kwamba wazazi wa mke wangu wananikosesha amani katika ndoa yangu kwa tabia yao na kuniombaomba pesa. Mara nyingi wanazonipigia simu huwa wanataka pesa tu. Nawaheshimu kama wakwe zangu lakini tabia yao hiyo inaniudhi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa umekuwa ukimlipia mke wako mahari kuambatana na makubaliano kati yako na wazazi wake. Kama ndivyo, tabia ya wakwe si nzuri na hata inaweza kusababisha migongano kati yako na mke wako. Kama mke wako ana hisia sawa na zako kuhusu wazazi wake, unaweza kumtuma ashauriane nao kuhusu suala hilo

Niko tayari kumuoa lakini nahisi kama ana wengine kando

SHANGAZI nina umri wa miaka 23 na kuna msichana ambaye niko tayari kumuoa. Hata hivyo naona ni kama ana uhusiano na wanaume wengine kwa sababu hajawa akinionyesha mapenzi ya dhati. Je, nimuache ama nifanye nini?

Kupitia SMS

Sielewi unamaanisha nini ukisema hajawa akikuonyesha mapenzi ya dhati. Pili, inaonekana unadhania tu wala huna hakika ana uhusiano na wanaume wengine. Badala ya kukaa kimya tu huku ukimshuku, ni heri uketi chini naye mjadili suala hilo ili ujue hasa msimamo wake.

Nahofia mjakazi atapindua serikali ya mwajiri wake

KWAKO shangazi. Nimeoa na mke wangu alipata mtoto wa kwanza hivi majuzi na ikabidi aajiri mjakazi ili kumsaidia kwa kazi za nyumbani. Tatizo ni kuwa ameajiri msichana aliyekomaa na mrembo hata kumshinda. Mgeni asiyemjua mke wangu akija nyumbani kwetu atadhani mjakazi ndiye mwenye nyumba. Nahofia akiendelea kuishi kwetu nitamkosea mke wangu na sitaki. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kupitia kwa maelezo yako, umefichua udhaifu wako ambao labda mke wako haujui – kwamba wewe ni mwanaume mnyonge kwa wanawake warembo. Huo ni udhaifu mbaya, kwani, mbali na mjakazi wenu huyo, unaweza pia kunaswa kwa haraka na mwanamke mwingine yeyote mrembo, wakiwemo majirani zenu. Kwa hivyo, kumfukuza kijakazi wenu si dawa. Suluhisho ni wewe urekebishe mtazamo wako kwa kukubali kuwa umeoa na kuheshimu ndoa yako.

Ni makosa kuwa na uhusiano ilhali wazazi ni marafiki?

HUJAMBO shangazi? Nimekuwa na uhusiano na kijana tunayeishi mitaa jirani. Sasa nimegundua kuwa baba yake na baba yangu ni marafiki wakubwa. Je, kuna makosa tukiwa wapenzi?

Kupitia SMS

Urafiki wa wazazi wenu hauwezi kuathiri kwa vyovyote uhusiano wenu wa kimapenzi. Badala yake, urafiki wao unafaa kuchochea zaidi uhusiano wenu kwa sababu wakati ukifika kwenu kufunga ndoa haitakuwa vigumu kwa kila mmoja wenu kumtambulisha mwenzake kwa baba yake kwa sababu tayari wanajuana.

 

 

Marafiki wa mpenzi wanamchochea aniache

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Saturday, January 20  2018 at  18:03

Kwa Muhtasari

Mpenzi wangu amebadili ghafla mipango yetu ya ndoa baada ya kushauriwa na marafiki zake atafute mwanamume mwenye kazi nzuri kwa sababu mimi ni kibarua tu; nishauri.

 

SHANGAZI AKUJIBU

Marafiki wa mpenzi wanamchochea aniache

VIPI shangazi? Mpenzi wangu amebadili ghafla mipango yetu ya ndoa, sasa hanitaki tena. Kisa ni kwamba ameshauriwa na marafiki zake atafute mwanamume mwenye kazi nzuri kwa sababu mimi ni kibarua tu. Nampenda sana, sijui nifanye nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi sababu ya mwenzako kubadili nia yake ghafla kama kweli anakupenda kwa dhati. Inaonekana yeye pia amekuwa katika uhusiano huo shingo upande kwani ana haki ya kujiamulia anachotaka maishani hata bila kushawishiwa na marafiki. Kama ameshamua kukuacha itabidi ukubali uamuzi wake.

Maisha ya ndoa ni sawa na jehanamu!

SHANGAZI nimeoa lakini wakati mwingine hujuta kwamba nilioa mke niliye naye. Sababu ni kwamba ni msumbufu sana, sina amani kabisa nyumbani ni kama kwamba naishi jehanamu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni kweli ndoa inaweza kugeuka jehanamu inapokuwa yenye mateso na dhuluma. Wakati mwingine ni vyema kwa wahusika kukabili ukweli kwamba hawawezi kuishi pamoja na kuachana roho safi. Mwelezee mke wako unavyohisi na pia umshauri kuhusu talaka.

Bila shaka ananitaka

KWAKO shangazi. Kuna mrembo ambaye amenasa moyo wangu na inaonekana yeye pia ana hisia kwangu kwani tunapokutana hunichangamkia sana utadhani tumejuana kwa muda mrefu. Nishauri.

Kupitia SMS

Tunaambiwa kuwa mapenzi ni kikohozi hayafichiki. Kutokana na maelezo yako ni wazi kuwa umeona dalili za mwenzako kuvutiwa kwako kimahaba. Hatua unayofaa kuchukua sasa ni kumdokezea hisia zako ili naye apate nafasi ya kuungama iwapo anahisi vivyo hivyo.

Nahofia dada yangu atatumiwa atemwe

MAMBO shangazi. Nimegundua kuwa dada yangu ameshikana na mwanamume ambaye ninajua ana msururu wa wasichana na nina hakika anataka kumtumia tu. Nahofia kumwambia kwani sijui kama atanisikiza ama atasema ninaingilia maisha yake binafsi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sidhani ungependa kuacha dada yako aendelee kutumiwa vibaya na mtu ambaye unajua kwa hakika hana mienendo mizuri. Ni muhimu umwambie ili aweze kufanya uamuzi wake kuliko ukose kumwambia kisha uje kujuta baadaye akifikwa na mabaya.

Ameahidi kumuacha mkewe kisha anioe

SHIKAMOO shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamume ambaye ameoa. Amekuwa akiniambia hana raha katika ndoa yake na anapanga kumtaliki mkewe kisha anioe. Hata hivyo, nimechunguza na sioni dalili zao kuachana kwani wanaishi tu kwa furaha. Nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo ni muongo na anataka tu muendelee na uhusiano wa kando kwa manufaa yake. Kama kweli hana furaha katika ndoa yake angekuwa ameanzisha utaratibu wa talaka. Usikubali kuendelea kutumiwa kwa ahadi zisizo na msingi.

Nilikosea kutoboa siri ya mume wa rafiki?

KWAKO shangazi. Nina rafiki yangu ambaye mumewe amekuwa akitembea na wanawake wengine mtaani ingawa yeye hajui. Juzi nilimfumania katika maskani ya burudani na nikampigia simu rafiki yangu kumwambia. Alikuja wakagombana sana na tangu hapo ananichukia sana nahofia anaweza kunidhuru. Je, nilikosea?

Kupitia SMS

Hata kama mwanamke huyo ni rafiki yako, nahisi ulikiuka mipaka kwa kitendo chako hicho kwani hata unaweza kuwafanya wavunje ndoa yako. Kuna usemi kuwa pilipili usiyoila haifai kukuwasha. Ndoa ni jambo la kibinafsi kati ya wahusika na ni makosa kwa watu wengine kuingilia.

Naogopa tutaoana kisha mkewe arudi

KUNA mwanaume tunayependana na tumekubaliana atanioa. Lakini nimesikia alikuwa na mke na wakaachana. Sasa naogopa huenda mke wake akarudi na kunipata kwake. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Badala ya kutegemea habari za kuambiwa, ni muhimu umuulize mwanaume mwenyewe. Kama kweli alikuwa na mke, thibitisha kutoka kwake na ikiwezekana kutoka kwa jamaa na marafiki zake kwamba wameachana kabisa na hakuna matumaini kwao kurudiana.