Ni zamu ya Dk Mwinyi bungeni

Na Ibrahim Yamola

Imepakiwa - Monday, May 14  2018 at  12:03

Kwa Muhtasari

Ile dhana ya zamani ya Jeshi la Wananchi kuwa chombo cha wananchi isimamie hilo na kuepuka kuliingiza jeshi katika mambo ya kisiasa na wajikite kulinda amani ya nchi na mipaka yake,”

 

 

Dodoma. Kikao cha 28 cha mkutano wa 11 wa Bunge kinaendelea leo jijini Dodoma ambako pamoja na mambo mengine kitajadili na kupitisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka 2018/19.

Wizara ya Ulinzi ni ya 13 kati ya 21 za Serikali zinazowasilisha bajeti tangu kuanza kwa mkutano huo Aprili 3, ukitarajiwa kumalizika Juni 26.

Zimebaki wizara nane ukiacha bajeti kuu ya Serikali itakayosomwa Juni 14.

Wizara zilizosalia ni Kilimo; Mifugo na Uvuvi; Maliasili na Utalii; Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa; Nishati; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Madini; na Fedha na Mipango.

Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi hatarajiwi kukutana na kashikashi za wabunge kama ilivyokuwa kwa mawaziri waliotangulia kuwasilisha bajeti zao kutokana na mazingira ya wizara anayoiongoza.

Ingawa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itaendelea kutowasilisha maoni yake kuhusu bajeti zake, lakini msemaji kwa wizara hiyo, Mwita Waitara alipozungumza na Mwananchi jana alisema kikubwa kinachopaswa kufanyika ni kuboresha masilahi ya wanajeshi.

“Ile dhana ya zamani ya Jeshi la Wananchi kuwa chombo cha wananchi isimamie hilo na kuepuka kuliingiza jeshi katika mambo ya kisiasa na wajikite kulinda amani ya nchi na mipaka yake,” alisema.

Waitara ambaye pia ni mbunge wa Ukonga (Chadema) alisema anatarajia kuona bajeti ikiboresha masilahi ya wanajeshi ambao kazi wanayofanya ni kubwa na Serikali inapaswa kuangalia kwa kina na undani mazingira yao.

“Yale maduka ya kutoa huduma kwa wanajeshi yanapaswa kuwapo ili kuwawezesha kupata huduma kwa urahisi na hasa kutokana na bidhaa zao kuwa zinaondolewa kodi, natarajia waziri kesho (leo) atalizungumzia hili,” alisema.

Alisema kumekuwapo madai ya wanajeshi wanaostaafu kutolipwa kwa wakati.

“Hili nalo linapaswa kuangaliwa na kuwalipa kwa wakati kwa kuwa wanakuwa wameitumikia nchi kwa uadilifu mkubwa,” alisema.

Akiizungumzia wizara hiyo, mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mussa Sima aliishukuru Serikali kwa kuliwezesha jeshi kuendelea kuwa imara na kulinda nchi na mipaka yake.

Sima alisema kutokana na kazi kubwa inayofanywa na wapiganaji, masilahi yao yanapaswa kuangaliwa kwa ukaribu na kuboreshwa, yakiwamo makazi yao.

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema, “Amani tuliyonayo ni kwa sababu ya jeshi imara, ulinzi wa mipaka yetu umeendelea kuwa imara lakini, tunapaswa kubadili mifumo yetu ya kiulinzi ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, tuwe na vifaa vya kisasa vya ulinzi.”