http://www.swahilihub.com/image/view/-/4566764/medRes/1976249/-/145tp5v/-/gesi+pic.jpg

 

Ipo tofauti ya gesi iliyosindikwa na ile ya mabomba

 

Na Beatus Rwechungura

Imepakiwa - Thursday, May 17  2018 at  15:58

Kwa Muhtasari

Gesi asilia ni rasilimali yenye thamani kubwa na itaendelea kuwa muhimu zaidi kwa nchi nyingi kwa miongo kadhaa ijayo zikiwamo Tanzania na Msumbiji.

 

Gesi asilia ni rasilimali yenye thamani kubwa na itaendelea kuwa muhimu zaidi kwa nchi nyingi kwa miongo kadhaa ijayo zikiwamo Tanzania na Msumbiji.

Si tu inaweza kuzalisha nishati ya gharama nafuu na yenye ufanisi, bali ina kiwango kidogo cha uchafuzi wa wa mazingira inapotumika, hivyo kuwa rafiki wa mazingira ikilinganishwa na nishati nyingine kama vile makaa ya mawe, kuni na mkaa

Hii inamaanisha gesi asilia ni chanzo muhimu cha nishati wakati dunia ikihangaika kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa.

Kwa muda mrefu, gesi asilia imekuwa ikitumiwa na nchi zilizo karibu na hazina hiyo, kwani imekuwa ni lazima kuisafirisha kutoka kwenye chanzo hadi mtumiaji wa mwisho kupitia mabomba yaliyojengwa ardhini.

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo na mabadiliko. Maendeleo ya teknolojia ya LNG yameongeza kwa kiwango kikubwa uwezo wa gesi asilia kuzalisha nishati kwa nchi nyingi duniani kote kwa sababu sasa inaweza kusafirishwa.

Gesi asilia na nishati nyingine zitokanazo na visukuku au mabaki ya mimea na wanyama zinaweza kupatikana katika kina kirefu chini ya ardhi, na ni matokeo ya mimea na wanyama waliokufa hatimaye kuoza mamilioni ya miaka iliyopita.

Katika kipindi hicho, matabaka mengi ya mchanga, miamba na tope yalijengeka juu ya mabaki haya ya viumbe hai na kutokana na mchanganyiko huo, joto na mgandamizo yaligeuka kuwa ama mafuta ya petroli, makaa ya mawe au gesi asilia.

Aina hizi tatu zinajulikana kama ‘nishati za visukuku’ na zimetumika kwa mamia ya miaka kupikia chakula, kuleta joto majumbani na kuzalisha nishati kwa matumizi mbalimbali.

Kwa vile gesi asilia inapatikana katika kina kirefu chini ya usawa wa ardhi, wakati mwingine inakuwa ni vigumu sana kujua kwa uhakika mahali ilipo. Utafiti wa mitetemo mara nyingi hufanywa na wataalamu wa jiolojia kujua iwapo eneo fulani lina uwezekano wa kuwa na gesi na baada ya hapo visima vya ugunduzi vinachimbwa ili kuthibitisha iwapo kweli ipo ama la.

Mara nyingi maeneo haya hupatikana chini ya bahari, hivyo kuzalisha na kusafirisha gesi hiyo inaweza kuwa na changamoto za usafirishaji na vifaa ambavyo hata hivyo ni ghali.

Uwekezaji mkubwa, kwa ujumla kutoka serikalini au kampuni kubwa za nishati duniani, mara nyingi huhitajika kuzalisha gesi hiyo. Mchakato wa kupata uwekezaji huu huchukua muda mrefu na teknolojia inayohitajika kwa miradi hii inaweza kuchukua miezi kama si miaka kuijenga.

Kwa ujumla, mabomba ndio njia ya ufanisi zaidi ya kusafirisha gesi asilia nchi kavu kwa umbali mfupi. Mabomba huchukua gesi kutoka kwenye mitambo inayoichakata na huisambaza majumbani, maeneo ya biashara na kituo chochote kinachohitaji nishati.

Imewezekana kusafirisha gesi asilia kwa kutumia mabomba kwa miaka mingi, lakini njia hii ina udhaifu mkubwa wa aina mbili.

Kwanza, hili linawezekana nchi kavu pekee. Wakati inawezakana kinadharia kuvuka bahari, mara nyingi kuna ugumu na ni gharama kubwa. Pili, mabomba yana gharama kubwa kuyanunua na kuyatandaza kwa kila kilomita bila kujali uwezo na kipenyo cha bomba, lakini kwa ujumla yana gharama za chini za uendeshaji.

Matokeo ya hili ni kwamba, wakati kuna faida kusafirisha gesi kwa bomba katika umbali mfupi, kugharamia usafirishaji kwa umbali mrefu ujazo mkubwa unahitajika kufanya shughuli nzima iwe na faida.

Kwa mfano, bomba la gesi kutoka Siberia nchini Urusi ambalo hupeleka gesi Ulaya limeweza kufanikiwa kwa sababu ya uwezo wake mkubwa na saizi ukichukulia Ulaya ni soko kubwa la kutosha na kwamba gesi yote inaweza kutumika.

Kwa bahati nzuri kwa siku hizi, gesi asilia iliyosindikwa (LNG) inaweza kutatua matatizo yote haya. LNG, kwa maana yoyote ile, ni gesi asilia iliyogeuzwa kuwa kimiminika. Hii huifanya iwe salama zaidi kwa sababu sio rahisi kushika moto, hivyo inaweza kusafirishwa kwenda nchi za mbali bila madhara.

Gesi asilia inapogeuzwa kimiminika hupungua ujazo wake mara 600. Hii ina maana kwamba kiasi kikubwa kinaweza kuhifadhiwa katika meli zilizojengwa mahsusi kwa shughuli hiyo, hivyo kusafirishwa sehemu mbalimbali duniani.

Aidha, LNG hufanya kazi katika viwango vidogo. Marekani na Japan zimeanzisha teknolojia hii tangu miaka ya 1990 na hivi karibuni Tanzania imefuata mkumbo.

Tanzania kwa sasa ipo mahali itakapoweza kunufaika kwa kiasi kikubwa na LNG na gesi asilia kutokana na hazina yake kubwa ya zaidi ya futi trilioni 57 za ujazo.