http://www.swahilihub.com/image/view/-/4568198/medRes/1977248/-/47kyg2z/-/twa+pic.png

 

Wengi wako tayari kulipia ada wakihakikishiwa elimu bora

Mkurugenzi mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyekuze akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti ya utafiti wa elimu 

Na George Njogopa

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  12:24

 

Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Twaweza na matokeo yake kutolewa jana unaonyesha kuwa asilimia 87 ya Watanzania wanataka kiwango cha elimu kiboreshwe na wapo tayari kulipia ada ilimradi elimu hiyo itoe mafanikio.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mkurugenzi mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema wazazi wengi wanataka elimu iliyo bora na wameonyesha wako tayari kuigharimia.

“Wananchi tisa kati ya 10 wanasema ni bora tukaongeza viwango vya elimu hata kama italazimu kulipa ada. Utafiti huu umebaini kwamba ni wazazi wachache sana huzingatia ada nafuu ambao ni asilimia sita na umbali wa shule asilimia 18 wakati wa kuchagua shule za sekondari kwa ajili ya watoto wao.”

“Badala yake wazazi wengi huzingatia zaidi viwango vya juu vya ufaulu wa shule husika na walimu wanaojituma,” alisema Eyekuze.

Eyakuze alisema kumekuwa na idadi ya kuridhisha ya wazazi kupenda kuchangia miradi itakayosaidia shule kuendelea kimasomo. Alisema kulingana na utafiti huo, mitazamo ya wananchi imeonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa na imetokana na kiu yao ya kutaka mabadiliko kwenye mfumo wa elimu.

Hata hivyo, alisema tangu Serikali ianze kutekeleza sera ya elimu bila malipo kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa shuleni jambo ambalo limesababisha changamoto nyingi.

Kuhusu matokeo hayo, Mwalimu Othiniel Mnkande alisema hakuna mzazi anayeshindwa kugharimia kusomesha watoto lakini inapojitokeza shule zilizopo zinashindwa kutoa matokeo mazuri hufanya wazazi hao kuwa na chaguo jingine.

“Tatizo si umaskini, bali hiyo elimu ina msaada gani kwa jamii... elimu yetu lazima itambue watoto wenye uwezo mdogo, kati na mkubwa lakini kama tutaendelea kuwaweka katika tabaka moja hatufiki mbali,” alisema.

Michango ya wadau

Wakizungumza wakati wa kujadili ripoti ya utafiti huo uliopewa jina la Elimu Bora au Bora Elimu? Elimu waitakayo wananchi wadau wa elimu waliungana na marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kuhusu hali ya elimu na kutaka mjadala wa kitaifa.

Marais hao katika nyakati tofauti wamewahi kuibua hoja juu ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu na Mkapa alipendekeza kuwapo mjadala wa kitafa utakaoangazia namna bora ya kuliokoa Taifa dhidi ya janga hilo huku Kikwete akizungumzia hali ya elimu barani Afrika akisema inahitaji mjadala.

Mbunge wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk Perpetua Nderakindo alisema akiangalia mazingira ya elimu yalivyo, anakubaliana na hoja za viongozi hao kuhusu kuwepo mjadala wa elimu.

Dk Nderakindo akitoa mfano wa kauli ya Mkapa, alisema inathibitisha mfumo wa elimu jinsi ulivyo na kasoro na kupendekeza njia ya kuondokana na tatizo hilo kuwa ni kwa Taifa kujitoa kwenye mfumo huo na kisha kuanza kuutazama upya.

“Rais Mkapa hakuwahi kuzungumzia suala hilo wakati alipokuwa madarakani lakini ametoka amezungumza kwa nini alishindwa... kulikuwa na kitu kinawabana,” alisema.

“Sisi kama Taifa bado hatutambui tupo katika mfumo wa aina gani na njia pekee ya kuondokana na mkanganyiko huo ni kutoka kwenye mfumo uliopo na kuanza mjadala utakaotupeleka katika mwelekeo sahihi.”

Hoja ya ujira mdogo wanaopewa walimu na kutothaminiwa kwa kazi zao pia ilijitokeza kwenye mjadala huo, wachangiaji wengi wakisema hali hiyo imefanya walimu wakose morali na ari ya kufanya kazi.

Akitaka walimu wathaminiwe zaidi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Shukia alisema mamlaka husika ziongeze nguvu kuboresha elimu kwa kutengeneza mpango utakaowezesha wazazi kuendelea kuchangia elimu.

“Kwanza tuwawezeshe walimu lakini pia tutengeneze mkakati utakaotekelezwa kwa awamu ili wananchi waendelea kuwa sehemu ya kuchangia elimu maana ubora wa elimu hauwezi kuja kwa siku moja tu,” alisema.