http://www.swahilihub.com/image/view/-/4568560/medRes/1028186/-/2vqyopz/-/anc+pic.jpg

 

JPM aomba majina wadaiwa JWTZ

 

Na Kalunde Jamal

Imepakiwa - Friday, May 18  2018 at  15:04

 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa taasisi za Serikali na watu binafsi wanaodaiwa jumla ya Sh41.4 bilioni na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kulipa, huku akitaka apatiwe majina yao.

Alitoa agizo hilo jana akizindua kituo cha uwekezaji cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) baada ya maombi ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo kwamba amsaidie ili yalipwe.

Jenerali Mabeyo alisema changamoto waliyonayo ni kutolipwa kwa wakati madeni wanayowadai watu binafsi na taasisi za umma.

Baadhi ya malipo wanayodai ni ya kazi za ulinzi inayofanywa na Suma Guard, zaidi ya Sh3.4 bilioni. Pia, wanadai Sh38 bilioni za matrekta waliyotengeneza na kuyatoa kwa mkopo.

“Waziri wa ulinzi, katibu mkuu wa wizara waandikieni barua na mnitumie nakala ili niwe nafuatilia watakapokuwa wameanza kulipa. Nataka fedha hizo zipatikane ili ziweze kutumika kujenga viwanda vingine,” alisema Rais Magufuli akijibu maombi hayo.

“Mtu anaanzaje kuacha kulipa fedha ya Jeshi, hii ni dharau kubwa...” alihoji Rais.

Aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuanza kuwasaka wadaiwa hao akisema, “Kukopa harusi kulipa matanga, mimi ninataka iwe kukopa harusi na kulipa harusi pia.”

Alisema ziandikwe barua kwa taasisi zinazodaiwa na Suma Guard hata ikiwa ni Ikulu zipelekwe kwa ajili ya kufanya malipo.

Mbali ya agizo hilo, Rais Magufuli aliagiza apelekewe majina ya maofisa waandamizi wa JWTZ wastaafu ili awateue kwenye bodi akisema kila anapowaona bado ni vijana na wana uadilifu na nidhamu ileile.

“Nileteeni majina yao kwani napata shida kuteua viongozi wa bodi kutokana na tatizo la uadilifu wao. Lakini hawa bado wana uadilifu na nidhamu ya kutosha na bado ni vijana ambao sidhani kama yupo atakayekataa nikimteua atusaidie,” alisema.

Kuhusu kituo cha uwekezaji alichokizindua, Rais alisema nchi nyingi zimefanikiwa kwenye viwanda, sayansi na teknolojia kwa kuanzia jeshini akitoa mfano wa Misri yenye viwanda vikubwa 10 vya jeshi na Ethiopia yenye tisa.

“Nimefurahi kuja kuzindua kiwanda cha ushonaji na cha maji hapa kwa kuwa kitapunguza upotevu wa fedha za kigeni zilizokuwa zikipotea kutokana na kuagiza nguo kutoka nje ya nchi.”

Alisema majeshi yakishirikiana katika ujenzi wa viwanda kutokana na weledi, utaalamu, na uzalendo wao Tanzania itafanikiwa kwenye azma yake ya viwanda.

Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi alisema uzinduzi wa kituo hicho cha uwekezaji umeonyesha shauku ya jeshi ya kuunga mkono kikamilifu azma ya kuwa na Tanzania ya viwanda.

Alisema wizara ilikuwa inazungumza na wawekezaji kutoka Misri ambao walitembelea nchini wakati wa ziara ya Rais wa nchi hiyo, Abdel Al-Sisi, Agosti mwaka jana.

“Mazungumzo yanaendelea vizuri. Tunapanga kuanzisha kiwanda cha dawa na cha usindikaji wa nyama kwa ushirikiano kati yetu,” alisema Dk Mwinyi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alisema kiwanda cha maji kilichofunguliwa ni cha 68 nchini na kinazalisha ajira 6,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja 50,000.

ka kituo cha Mgulani ikiwa ni pamoja na; Kiwanda cha Mgulani National Service Garment, kiwanda cha maji safi ya kunywa, kumbi mbili za mikutano na sherehe, Shule ya Sekondari ya Jitegemee na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi.