http://www.swahilihub.com/image/view/-/4574120/medRes/1981441/-/vhgdeu/-/uju+pic.jpg

 

Kaa chonjo na sms zinazoelekeza kutuma fedha

 

Na Kalunde Jamal

Imepakiwa - Tuesday, May 22  2018 at  10:34

Kwa Muhtasari

Ukiona ujumbe wa ajabuajabu kwenye simu yako toa taarifa Polisi, usisubiri hadi utapeliwe

 

Dar es Salaam. Utapeli unaohusisha miamala ya fedha kupitia simu za mkononi umeshika kasi nchini, huku baadhi ya wahusika wakitumia kigezo cha uganga wa kienyeji.

Baadhi ya watumiaji wa simu waliozungumza na Mwananchi wameeleza kuwa wamekuwa wakipokea ujumbe mfupi wa maneno (sms) wakitakiwa kutuma fedha kwa namba wasizozijua.

Azzi Jabir, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam alisema hakumbuki kumpa namba yake mtu tofauti na jamaa zake, lakini anashangazwa kila mara hupokea ujumbe ukimtaka kutuma fedha kwa namba tofauti za simu.

“Nawalaumu wafanyakazi wa kampuni za simu, wapo wasio waaminifu ambao hutoa namba za wateja kwa matapeli,” alidai Jabir.

Mkazi mwingine wa Upanga jijini Dar es Salaam, Mwajuma Makilai alisimulia mkasa wa utapeli akisema hilo lilimfika baada ya kutoa taarifa zake wakati wa kazi ya kuzifunga simu bandia, hivyo kwa sasa kila ujumbe anaoupata anautilia shaka.

Mwajuma alisema laini yake ya mtandao wa Vodacom ndiyo hupokea zaidi ujumbe kuhusu mafanikio ya mtu aliyetumia dawa za mitishamba na kupata utajiri.

“Nimekuwa makini, lakini kuna rafiki yangu anafanya biashara kutokana na hali ngumu na kukosa wateja, aliingia mkenge wa ujumbe kama niliotumiwa na akatapeliwa,” alisema.

Alisema kupitia sms aliyotumiwa rafiki yake, aliwapigia simu wahusika waliomtaka awatumie fedha kwa ajili ya ununuzi wa mbuzi watatu wa kafara na vifaa vingine.

Kwa mujibu wa Mwajuma, rafiki yake alitoa Sh800,000 kwa watu hao na walipoachana kila alipopiga tena simu hawakupatikana.

Mkazi mwingine Zacharia Samson, alisema sms za utapeli zimekuwa kero kwa watumiaji wa simu, hivyo alishauri kampuni za simu kuliona hilo kama tatizo na kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo.

Akizungumzia sms hizo, meneja uhusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema wao hawahusiki.

Alisema wanaotumiwa ujumbe wanatakiwa kulalamikia kwa mamlaka husika ambazo ni ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Polisi. “Tunachofanya ni kuwaambia wateja wetu watumie simu kwa tija na kuepuka kujishughulisha na ujumbe wasioufahamu au kuwahusu hata kama umetumwa kwenye simu zao,” alisema Mmbando.

Meneja mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alipoulizwa kuhusu suala hilo, alimtaka mwandishi wa habari kuandika maswali ambayo hata hivyo hakuyajibu.

Kaimu meneja uhusiano wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema hawana jukumu kisheria la kushughulika na uhalifu wa mitandao.

Alisema wanachofanya ni kushirikiana na kitengo kinachofanya shughuli hiyo kilichopo Polisi (cybercrime) kufanya uchunguzi kiteknolojia.

“Kama kuna kesi inahitaji uchunguzi wa kiteknolojia, tunashirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha uhalifu wa mitandao tofauti na hapo hatuna haki wala sheria ya kushughulikia suala hilo,” alisema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema suala la kutoa elimu kuhusu utapeli wa njia ya simu siyo la Polisi peke yake.

“Taasisi za dini, wanasiasa wote wana wajibu wa kutoa elimu kuhusu suala hili kwa sababu limeshamiri,” alisema Mwakalukwa.

“Tunasema ukiona ujumbe wa ajabuajabu kwenye simu yako toa taarifa Polisi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine hao matapeli watapatikana, usisubiri hadi utapeliwe.”

Alipoulizwa suala hilo, mkuu wa mawasiliano wa Vodacom, Jacqueline Materu aliahidi kutoa majibu, lakini hakufanya hivyo.