Polo afutwa kwa kumtongoza mke wa bosi wake

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Sunday, January 10  2016 at  13:17

Kwa Muhtasari

Kalameni anayefanya kazi kwenye kampuni moja mjini hapa alijipata pabaya alipopigwa kalamu kwa kumtania kimapenzi mke wa bosi wake.

 

ELDORET MJINI

KALAMENI anayefanya kazi kwenye kampuni moja mjini hapa alijipata pabaya alipopigwa kalamu kwa kumtania kimapenzi mke wa bosi wake.

Jamaa alikuwa mhasibu kwenye kampuni hiyo na inasemekana kila kipusa aliyeingia katika ofisi yake, alikuwa akimrushia mistari ya mapenzi bila kujali alikuwa kazini.

“Jamaa ana tamaa ya fisi, hakuna kidosho aliyeenda kwenye ofisi yake na kutoka bila kumwachia nambari zake za simu na kumtania kimapenzi,” alieleza mdokezi.

Kulingana na penyenye, polo alikuwa akionywa dhidi ya tabia hiyo lakini hakusikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini.

Siku ya kisanga, mke wa mkurugenzi alizuru kazini bila kuarifu yeyote. Alipofika alianza kukagua kila kitengo kuanzia ofisi ya uhasibu.

“Jombi aliona kipusa aliyemzuzua na akaanza kumrushia mistari ya mapenzi kwa utani alivyozoea,” alisema mdokezi. Kalameni hakutaka kujua aliyemtania ni nani na sababu iliyompeleka kwenye ofisi yake.

“Hallo msupa, umeumbwa  kweli kweli. Ni Mungu  aliyekuleta kwangu na nakwambia pesa ninazo.

Mimi ndiye meneja wa uhasibu kwenye kampuni hii, nakualika tuponde raha pamoja,” alifoka polo akisimama na kumkaribia mke wa bosi na kujaribu kumpapasa.

Inasemekana mke wa bosi alitoka kwenye ofisi hiyo hadi kwa meneja wa uajiri  kumuita ashuhudie kioja hicho.

 “Hii ndiyo kazi inayofanyika huku? Hamna hata heshima kwa wageni wanaofika huku. Huduma za huyu jamaa zimeisha leo, simhitaji kamwe” alichemka mama huyo.

Kalameni alipojua  huyo  alikuwa mke wa mwenye kampuni, tayari maji yalikuwa yameshamwagika na hayangezoleka.

Juhudi zake za kuomba msamaha ziligonga mwamba kutokana na kitendo cha aibu alichofanya. Polo alifunganya virago vyake na kuacha ofisi ya mwenyewe alivyoipata.