Jombi atupwa jela kwa kuua mbwa wa mdosi

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Sunday, January 10  2016 at  13:37

Kwa Muhtasari

Kalameni mmoja eneo hili alishtuka baada ya kurushwa korokoroni kwa madai ya kumuua mbwa wa mdosi wake.

 

KAHAWA SUKARI, NAIROBI.

KALAMENI mmoja eneo hili alishtuka baada ya kurushwa korokoroni kwa madai ya kumuua mbwa wa mdosi wake.

Inasemekana kuwa polo aliajiriwa katika boma la mdosi huyo na kilichomkasirisha ni  hatua ya mdosi wake ya kumthamini mbwa kuliko yeye.

“Inakuaje mbwa awe wa maana  katika hili boma kumshinda binadamu? Eti mbwa analishwa  nyama ilhali mimi nala sukuma wiki.

Mbwa analala ndani ya nyumba na amenunuliwa godoro ilhali mimi sina. Haya hayawezekani,” polo alidokezea rafiki yake.

Inasemekana  jamaa aliamua kutafuta mbinu ya kumuua mbwa wa mdosi.

“Mdosi wa polo aliporejea kutoka kazini, alimpata mbwa wake akiwa marehemu na hasira zikampanda kwa sababu alimpenda mbwa huyo sana,” alieleza mdokezi.

“Haikosi ni wewe ulimuua mbwa wangu kwa sababu hakuna mtu mwingine hapa na  lazima utalala ndani,” boss alimkaripia  jamaa.

Kulingana na mdokezi, jamaa alikanusha vikali kumuua mbwa huyo lakini alipokuwa akipelekwa katika kituo cha polisi, ilibidi polo akiri makosa yake.

“Mimi nilimuua mbwa huyo kwa sababu unamthamini kushinda mwanadamu. Mbwa umempa jina la mwanadamu. Analala ndani ya nyumba, analishwa kwa nyama safi kuliko mimi. Huo ni ungwana kweli?” polo alimuuliza mdosi.