Polo afungiwa stoo kwa kuibia hoteli sukari

Na  TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Monday, January 11  2016 at  14:08

Kwa Muhtasari

Kalameni wa eneo hili, alijipata taabani baada ya kufungiwa stoo  siku nzima alipopatikana akiiba sukari katika hoteli.

 

MAILI SABA, Kitale

KALAMENI wa eneo hili, alijipata taabani baada ya kufungiwa stoo siku nzima alipopatikana akiiba sukari katika hoteli.

Kulingana na mdokezi, polo aliingia katika hoteli na kuketi karibu na meza iliyokuwa na bakuli iliyojaa sukari kisha akaagiza chai na andazi moja.

Inasemekana kuwa polo alianza kuweka sukari kwa chai huku akiweka nyingine katika mfuko wa long’i yake bila kujua weita mmoja alikuwa akimtazama.

Duru zasema alipokuwa akiondoka, weita alimsimamisha.

“Bosi, umekunywa chai vikombe vingapi?” weita huyo alimuuliza.

“Nimekunywa kikombe kimoja tu na ndicho ninalipia,” polo alimjibu weita. “Kwani kikombe kimoja ndicho kimemaliza sukari iliyokuwa imejaa kwenye hii sahani?” weita alimuuliza polo.

Inasemekana kuwa polo alianza kumzomea weita. “Sasa unafikiria mimi nimeramba sukari? Kwenda huko,” alisema.

Weita alimuagiza polo kutoa kila kitu kilichokuwa ndani ya mfuko  wa long’i yake na sukari ikapatikana ndani ya mfuko huo.

“Huyu jamaa nilikuwa nikiangalia alichokuwa akifanya. Mara tu alipoletewa chai, alijifanya aliumwa na kitu kumbe ni karatasi aliyokuwa akitoa kisha akaanza kuchota sukari na kuweka ndani ya hiyo karatasi,” weita alisimulia.

Ilibidi jamaa kupiga magoti na kuomba msamaha.

“Jamani mnisamehe. Sitarudia tena. Mimi ni kastoma wenu wa kila siku. Na tena najulikana hapa. Tafadhali msiniaibishe,” polo aliwarai wahudumu.

“Hakuna cha msamaha. Huyu jamaa lazima afungiwe hapa hadi bosi wetu aje,” weita mmoja aliwaeleza wenzake.

Inasemekana kuwa polo alipelekwa na kufungiwa katika chumba cha kuhifadhi vyakula. “Kaa huko mpaka upate adabu,” weita mmoja alisema huku akimsukuma polo ndani ya chumba na kumfungia ndani.