Aibu kwa mama kuhepesha hela za matanga

Na CORNELIUS MUTISYA

Imepakiwa - Tuesday, January 12  2016 at  15:20

Kwa Muhtasari

Mama wa hapa alipata aibu ya mwaka alipokamatwa baada ya kutoroka na pesa za chama cha mazishi.

 

KALUNGA, MACHAKOS

MAMA wa hapa alipata aibu ya mwaka alipokamatwa baada ya kutoroka na pesa za chama cha mazishi.

Inasemekana kuwa mama huyo aliyekuwa mweka hazina wa chama hicho alienda mafichoni lakini akasakwa na kulazimishwa kuzilipa.

Kulingana na mdokezi, mama huyo alichaguliwa mweka hazina wa chama cha mazishi kwa sababu aliheshimiwa na wakazi.Hakuna aliyedhani kuwa angebadilika na kutoroka na pesa za chama.

“Mama alichaguliwa na wakazi kuwa mweka hazina kwa sababu walimheshimu. Hakuna aliyedhani kuwa angetoroka na pesa hizo,’’ akasema mdokezi.

Inasemekna kwamba wanachama walichanga pesa kama ilivyokuwa desturi yao kila mwisho wa mwezi na kumkabidhi mweka hazina azipeleke benki.

Alipopewa hela hizo, badala ya kupeleka benki, aliamua kutoroka  hadi mjini Athiriver alikopanga chumba na kuanzisha biashara ya  mboga na matunda.

Penyenye zaarifu kwamba, wanachama waliingiwa na wasiwasi walipomkosa mama huyo kwa muda.Walishindwa kwa nini hakuwasilisha risiti ya benki kwa katibu wa chama ili aweke katika rekodi za chama.Walimtafuta kujua ukweli wa mambo.

“Mwenyekiti na katibu waliamua kwenda benki ili kuuliza baki ya akaunti yao. Walishangaa mno walipogundua kuwa mweka hazina hakuwa amepeleka pesa hizo benki,’’ akasema mdokezi.

Waliarifu wakazi ambao walianza kumsaka mama huyo na wakapata habari alikuwa akifanya biashara  mjini Athiriver.

Waliamua kumkabili ili awarejeshee hela zao.

“Walimwendea mama huyo mjini na wakamlazimisha arejeshe pesa za chama. Alikubaliana nao na akarejea nyumbani na kuuza ng’ombe kulipa pesa hizo.

Hata hivyo, aliondolewa kabisa kutoka wadhifa wa mweka hazina na akabaki mwanachama wa kawaida.’’ akasema mdokezi.

Duru zaarifu kwamba,  mama huyo hatoki nyumbani kwa sababu ya aibu.