Washangaa kugunua polo hupigwa na mke, si majambazi

Na CORNELIUS MUTISYA

Imepakiwa - Monday, January 18  2016 at  13:40

Kwa Muhtasari

Polo wa hapa aliwaacha wakazi vinywa wazi walipogundua kwamba aliwahadaa alikuwa amevamiwa na majambazi baada ya kutwangwa na mke wake.

 

KITHUNGUINI, MACHAKOS

POLO wa hapa aliwaacha wakazi vinywa wazi walipogundua kwamba aliwahadaa alikuwa amevamiwa na majambazi baada ya kutwangwa na mke wake.

Jamaa huyo alipiga nduru zilizowavutia wakazi na walipoenda kujua kilichojiri aliwafahamisha kwamba alikuwa amevamiwa na majambazi waliokuwa na silaha.

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa na mazoea ya kumpiga mkewe kila siku akimlaumu kwa makosa madogomadogo. Hali hii ilimfanya mkewe kukasirika na akazua njama ya kulipiza kisasi.

“Polo alikuwa na mazoea  ya kumpiga mke wake kila siku. Hali hii ilimfanya mama watoto kukasirika na akaamua kulipiza kisasi,” akasema mdokezi.

Inasemekana siku ya kioja, mama watoto alipika chakula mapema na akapakulia watoto kikaisha. Aliosha sufuria na akaketi sebuleni kumsubiri mumewe.

“Polo alipofika nyumbani mwendo wa saa tatu usiku, alianza kumwitisha mkewe chakula kwa fujo. Ugomvi ulizuka baina yao na mama watoto akachukua kipande cha ukuni na kumtwangwa mumewe kichwani,’’ akasema mdokezi.

Kulingana na mdokezi, polo alichomoka nje mithili ya swara aliyebumburushwa na akapiga kamsa akidai alikuwa ameshambuliwa na genge la majambazi waliojihami kwa silaha za kila aina.

Wakazi walifurika  kwake kumnusuru lakini wakashangaa walipopata  hakuwa amevamiwa na majangili kama alivyokuwa amedai.

Wakazi waliamua kufanya uchunguzi na wakagundua kuwa alikuwa ametwangwa na mkewe kwa kumsumbua akiitisha chakula ambacho hakununua.

“Wakazi walimuonya polo asithubutu tena kupiga kamsa akidai amevamiwa na wezi anakikosana na mkewe. Walimwambia anafaa kuketi chini na mkewe na kusuluhisha tofauti zao kwa njia ya kiutu uzima badala ya kumwaga mtama kwenye kuku wengi,’’ akasema mdokezi.

Inasemekana mkewe alisikika akimwambia kwamba hatavumilia dhuluma na akaapa kumwadhibu tena akiendelea kumsumbua.