Jombi sasa ni skwota baada ya kuuza shamba alipe mganga

Imepakiwa Saturday January 23 2016 | Na JOHN MUSYOKI

Kwa Muhtasari:

Polo amepiga kambi katika mitaa ya mji huu baada ya kukosa makao alipouza shamba lake ili amlipe mganga aliyemhudumia.

EMBU MJINI

POLO amepiga kambi katika mitaa ya mji huu baada ya kukosa makao alipouza shamba lake ili amlipe mganga aliyemhudumia.

Penyenye zasema kwamba jamaa aliamini familia yake ilikuwa imerogwa ikasambaratika na akaamua kutafuta huduma za mganga maarufu.

Inasemekana mganga huyo alifika na kufanya vituko vyake katika boma la jamaa huyo na kuahidi kwamba mambo yangekuwa shwari na  mke na watoto wake waliokuwa wamehama wangerudi.

Hata hivyo, badala ya mambo kuwa mazuri kwa jamaa, yaliendelea kuwa mabaya zaidi na akasita kumlipa mganga. Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa ameafikiana na mganga huyo kwamba angemlipa baada ya kuona matunda ya kazi yake.

“Lakini jamaa alikosa kuona mabadiliko katika muda ambao alikuwa ameahidiwa na mganga huyo. Fauka ya yote, alifutwa kazi hata kabla ya kipindi hicho kukamilika akawa hana mbele wala nyuma,” akasema mdokezi.

Inasemekana mganga alianza kumtisha jamaa angekiona cha mtema kuni asipomlipa na ikabidi auze shamba. Kwa sasa anahangaika mitaani akiombaomba sababu familia yae imemkataa.

Share Bookmark Print

Rating