Demu azua kizaazaa kilabuni kwa kuzaba mpenziwe makofi

Na JOHN MUSYOKI

Imepakiwa - Saturday, January 23  2016 at  14:12

Kwa Muhtasari

Kizaazaa kilizuka katika baa kipusa alipompiga mpenzi wake kwa kumpata akisakata densi na kidosho mwingine.

 

KITHIMANI, MACHAKOS

KIZAAZAA kilizuka katika baa kipusa alipompiga mpenzi wake kwa kumpata akisakata densi na kidosho mwingine.

Inasemekana kwamba mwanadada huyo alikuwa akishuku jamaa alikuwa na tabia ya kuburudisha vipusa wengine na akaamua kuchunguza ili kubaini ukweli.

Siku ya kisanga alimpigia jamaa simu wakutane kujivinjari lakini akamfahamisha alikuwa na shughuli nyingi na hangepata nafasi.

Mwanadada huyo alipata habari kutoka kwa makachero wake kwamba polo alionekana akiburudika na kipusa mwingine. Alipofika, aliwapata wakinengua viuno na bila kusita alimzaba jamaa makofi makali yaliyoshtua wateja wengine.

“Mwanamume malaya wewe. Ulidhani sitakupata, usiwahi kunikaribia tena,” kipusa alimfokea jamaa na kuondoka kwa hasira.