Polo asusia pilau akishuku ina sumu

Imepakiwa Sunday January 24 2016 | Na GRACE KARANJA 

Kwa Muhtasari:

Kioja kilizuka katika nyumba moja mtaani hapa  jombi aliposusia pilau akishuku kwamba viungo vilivyowekwa na mkewe vilikuwa sumu.

DANDORA, NAIROBI

KIOJA kilizuka katika nyumba moja mtaani hapa  jombi aliposusia pilau akishuku kwamba viungo vilivyowekwa na mkewe vilikuwa sumu.

Penyenye zaarifu kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwa mke wa jombi kuweka pilau masala kwa wali jambo ambalo lilimshtua.

“Jamaa alishtushwa na pilau masala kwa sababu mkewe hakuwa ameitia kwa wali hapo awali,” mdokezi alieleza.

Inasemekana kwamba wawili hao walikuwa waking’ang’ana na maisha kwa muda mrefu na ilikuwa tatizo kupika vyakula vya aina tofauti.

Usiku wa kioja, jamaa alitoka kazini kama kawaida na kupumzika kitini ili apikiwe na mkewe.

“Leo hutaamini chakula  nilichokupikia, ni pilau,” mkewe alimwambia jamaa.

Hapo ndipo alipoweka mezani sinia iliyojaa pilau na kumkaribisha mumewe ale.

Badala ya jombi kufurahia chakula, alimrudishia mkewe pilau na kumwambia kwamba ikiwa alikuwa na mpango ya kumuua siku hiyo, hangefaulu.

“Si ungesubiri tu niwe na mali kiasi ndio uniue ubaki nayo, mipango yako imesabaratika. Hicho chakula chako unachokiita pilau sikitaki.

Mbona wali umebadili rangi? Sitaki, kula mwenyewe, ndio maana umeweka nyama kwa sababu wajua naipenda,” jamaa alimfokea mkewe.

Kulingana na mdokezi, ilibidi mkewe kutafuna vijiko kadhaa na kuvimeza ili kumhakikishia mumewe chakula hakikuwa na sumu.

“Miaka hiyo yote nimekaa nawe mbona niamue kukuua leo. Hii ni pilau masala niliyoweka ili wali unukie vizuri. Kama huamini wacha nile vijiko kadhaa nife kwanza tuone,” mkewe alimweleza jombi.

Inasemekana kwamba jombi alimwomba mkewe msamaha kisha wakaendelea kula pamoja na bila hofu ya kuangamizwa.

Baadaye jamaa alimsifu mkewe kwa kumpikia chakula kitamu sana na mara kwa mara akawa anamuomba ampikie pilau.

Share Bookmark Print

Rating