Demu atemwa kwa kuzidiwa na tamaa

Imepakiwa Tuesday January 26 2016 | Na GRACE KARANJA

Kwa Muhtasari:

Mwanadada kutoka mtaa huu, hakuamini macho yake alipotemwa na mumewe kwa kuwa na tamaa ya kutaka kila kitu.

MAKONGENI, Thika

MWANADADA kutoka mtaa huu, hakuamini macho yake alipotemwa na mumewe kwa kuwa na tamaa ya kutaka kila kitu.

Duru zaarifu kwamba, wawili hao walikuwa wameishi katika ndoa kwa mwaka mmoja lakini kila mara walisikika wakigombana.

“Hawakuweza kukaa hata siku tatu bila kurushiana maneno. Ilikuwa ni mabishano, ugomvi na hasira,” mdokezi alisema.

Sababu ya ugomvi huo ilikuwa tabia ya mwanadada ya kumlazimisha mumewe kumfanyia mambo ambayo hangeyamudu.

Yasemekana  mumewe alikuwa amemuonya mara nyingi dhidi ya tabia ya kutamani maisha ya juu.

“Jamaa alikuwa amemwambia mkewe kwamba mambo hufanywa kwa mpango lakini hakusikia,” akasema mdokezi.

Jioni ya kisanga, jamaa alirudi nyumbani bila viatu ambavyo mwanadada alikuwa amemwitisha jambo lililomfanya mkewe kumfokea mbele ya majirani.

“Mbona leo hukuniletea chochote na uliniahidi viatu,” mwanadada alitaka kujua.

Swali hilo lilimkera sana jamaa na kumwambia mkewe kwamba alimkosea heshima mbele ya majirani.

“Nyamaza, unataka kuwajulisha majirani ndio wafanye nini? Ni mara ngapi nimekuonya dhidi ya kutaka maisha ya juu usiyoyaweza? Ni nini ambacho sijakununulia tangu nikuoe, una jozi ngapi za viatu hata zingine hata huvai? Sijui unata zingine za kupeleka wapi?

Mimi sikuapa kuishi maisha hayo na kuanzia dakika hii kwa sababu ya kuniabisha mbele ya majirani, kesho uamke uende utafute kazi uwe tajiri uweze kujipa chochote utakacho maishani,” jamaa alimwambia mkewe kwa hasira.

Hata hivyo, mwanadada huyo alichukulia matamshi ya jamaa kama mzaha tu na hakutilia maanani onyo hilo.

Kulingana na mdokezi, siku iliyofuata, jamaa aliamka na kumfukuza mwanadada huyo dhihirisho kwamba hakuwa akifanya mzaha alipomwambia alikuwa amechoshwa na tabia yake.

 

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com   

Share Bookmark Print

Rating