Polo amtandika mkewe kwa kupeleka hela kwao kisiri

Imepakiwa Tuesday January 26 2016 | Na  TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Kizaazaa kilizuka eneo hili baada ya polo kumwadhibu mkewe alipogundua kwamba alipeleka pesa alizonuia kujenga nyumba kwao kisiri.

GATUNDU, KIAMBU.

KIZAAZAA kilizuka eneo hili baada ya polo kumwadhibu mkewe alipogundua kwamba alipeleka pesa alizonuia kujenga nyumba kwao kisiri.

Penyenye zasema polo alimpa mkewe pesa hizo aziweke akiwa na mipango ya kuongeza zingine ili ajenge nyumba.

Lakini baada ya muda, polo aliona mienendo ya mkewe ikibadilika jambo

lililomtia wasiwasi mwingi sana.

Jamaa alimwambia mkewe ampe pesa hizo ili aanze kupanga mradi wake.

“Mama watoto ebu nipe zile pesa. Ninataka kumuita fundi juma lijalo ili aanze ule mradi niliokuambia,” polo alimueleza mkewe.

Duru zinasema mkewe  hakutoa pesa na akaamua kumweleza  mumewe ukweli kwamba alimpa mama yake pesa hizo.

“Unasema pesa ulimpelekea mama yako? You are jocking. Nakupa nusu saa uniletee hizo pesa. Kimbia kwenu uzilete,” polo alimwamuru mkewe.

“Kwani watu wa kwetu pia hawawezi kula chako? Acha kukaa mkono gamu. Hizo pesa zitatumika kama mahari,” mwanadada alimweleza mkewe.

Inasemekana polo alipandwa na hasira. “Eti mahari? Kwa hivyo hii nyumba ikianguka tutaenda kuishi kwenu?” polo alimuuliza mkewe kwa hasira.

Kulingana na mdokezi, jamaa alianza kumzaba mkewe makofi.

“Nimekwambia ukimbie kwenu uniletee pesa, alafu unaniangalia. Nataka pesa saa

hizi,” polo alimfokea mkewe.

Inasemekana mkewe  aliamua kulia kwa sauti na kuwavutia majirani.

“Mimi najikaza ili nimpe mke wangu maisha mazuri kisha nikimpa pesa aweke, anapeleka kwa wazazi wake  eti hiyo ni kama mahari. Tangu lini wanawake wakaanza kutoa mahari?” polo aliuliza majirani kwa hasira.

Kila mtu alibaki akicheka tu na kuwaacha wawili hao kusuluhisha mambo yao.

Mwishowe mwanadada alilazimika  kwenda kwao na haikufahamika ikiwa alimrudishia  mumewe pesa zake.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com   

Share Bookmark Print

Rating