Mbunge achomolewa pochi akipanda jukwaani

Na BENSON MATHEKA.

Imepakiwa - Tuesday, January 26  2016 at  14:13

Kwa Muhtasari

Mbunge mmoja nusura atokwe na machozi wachomozi walipotoweka na pochi lake alipokuwa akipanda jukwaani kujiunga na wanasiasa wenzake wakati wa mkutano wa hadhara.

 

MACHAKOS  MJINI

MBUNGE mmoja nusura atokwe na machozi wachomozi walipotoweka na pochi lake alipokuwa akipanda jukwaani kujiunga na wanasiasa wenzake wakati wa mkutano wa hadhara.

Mkutano huo uliohudhuriwa na vinara wa upinzani ulivutia umati mkubwa uliozunguka jukwaa.

Ni wakati mheshimiwa huyo alipokuwa akipanda jukwaani ambako mwanamuziki mmoja maarufu alikuwa akitumbuiza wachomozi walipata fursa ya kuchomoa pochi lake lililokuwa kwenye mfuko wa long’i yake.

Ingawa aling’amua kwamba pochi lake lilikuwa limechomolewa, mheshimiwa huyo alivumilia hadi mkutano ulipokamilika dakika chache kabla ya saa moja usiku ambapo alimwendea mwelekezi na kumfahamisha kilichokuwa kimetendeka.

“Jamani kuna tangazo hapa. Mheshimiwa huyu amepoteza pochi lake. Halina pesa, ni kadi za kibiashara na benki zilizo ndani.

Tafadhani ikiwa umechukua kipochi hicho mrudishie mheshimiwa, hautachukuliwa hatua zozote za kisheria. Tutakupatia zawadi ya Sh2000 ukipata kipochi hicho,” mwelekezi alitangazia watu ambao walikuwa wameanza kuondoka uwanjani.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com