Atwangwa kwa kupatikana ndani ya mzinga wa rafiki yake

Imepakiwa Friday January 29 2016 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Kalameni wa hapa nusura ajikatie tiketi ya bure  kwenda ahera alipofumaniwa akichovya asali ya mke wa rafiki yake.

GITHURAI 45, NAIROBI

KALAMENI wa hapa nusura ajikatie tiketi ya bure  kwenda ahera alipofumaniwa akichovya asali ya mke wa rafiki yake.

Jamaa huyo ni mhudumu wa teksi mtaani hapa. Kulingana na mdaku,  polo alifurusha mkewe miezi minne iliyopita ili aweze kuwa na uhusiano haramu wa kimapenzi na mama huyo.

Duru za kuaminika zinasema mke wa polo na mama huyo walikuwa marafiki wakubwa kabla ya kufurushwa. Hata hivyo, hakujua kwamba mumewe alikuwa akimnyemelea rafiki yake.

“Mke wa jamaa hakujua kilicho mla kilikuwa nguoni mwake,” alisimulia mdokezi wetu.

Minong’ono inasema kwamba  jamaa alitahadharishwa na watu aepuke uhusiano na mwanadada huyo lakini hakusikia la mwadhini wala la mteka maji msikitini.

Siku ya kioja, mwendo wa saa kumi na mbili hivi za jioni, kalameni alimualika mpango wake wa kando alikoegesha teksi yake na wakazama kwenye raha zao.

Yasemekana mume wa  mama huyo alifika nyumbani na kumkosa mkewe na alimpigia  simu  hakuijibu.

Aliamua kwenda kumsaka mkewe sokoni na kwa bahati jirani mmoja alimdokezea kwamba alimuona akiingia teksi ya polo.

Inasemekana kuwa alielekezwa polo alikoegesha teksi yake na kumpata akimumunyana na mkewe. “Polo aliangushiwa kichapo. Alipohisi mauti yakibisha hodi, alipiga magoti na kuomba msamaha,” akasema mdokezi.

“Ulifukuza mkeo ili uharibu wanawake wa wenyewe? Leo nitakufunza adabu iwapo hukufunzwa na mama yako ?”kalameni alichemka akihema kwa hasira huku mkewe akitimka mbio kama swara.

Polo aliokolewa na maafisa wa polisi waliopigiwa simu na watu waliofika kujionea sinema hiyo ya bure. Hadi wakati mdokezi alipotoka kwenye eneo la kioja hicho hakuna aliyejua alikoelekea mwanadada huyo mgawa asali.

Share Bookmark Print

Rating