Purukushani polo akilazimishwa kumpenda mkewe

Imepakiwa Friday January 29 2016 | Na GRACE KARANJA

Kwa Muhtasari:

Rabsha zilizuka katika boma eneo hili, jamaa alipolazimishwa na wazazi wake kuandamana na mkewe mjini baada ya kumtelekeza mashambani.

NDITHINI, THIKA

RABSHA zilizuka katika boma eneo hili, jamaa alipolazimishwa na wazazi wake kuandamana na mkewe mjini baada ya kumtelekeza mashambani.

Kulingana na mdokezi, jamaa hufanya kazi mjini na ni nadra sana kumtembelea mkewe mashambani.

“Tangu aoe alimuacha mkewe ocha, hamjali na alimaliza mwaka bila kumtembelea,” mdokezi alieleza.

Yasemekana  majuma mawili kabla ya tukio, mkewe alimpigia simu na kumfahamisha nia yake ya kutaka kumtembelea mjini lakini jamaa alikataa.

Hapo ndipo mkewe alipochukua hatua ya kuwaeleza wakwe zake.

“Mimi nimechoka kukaa hapa peke yangu. Ikiwa sikuolewa kama wanawake wengine nijulishwe mapema. Mpigieni simu mwana wenu aje kunichukua na kama hatafanya hivyo nitaenda zangu,” mwanadada alisema.

“Usiwe na hofu hata mimi siwezi kukubali ndoa kama hiyo. Nilipomuoa huyu mama yako sikumwachia wazazi wangu. Nilikwenda naye popote pale nilikuwa nikifanya kazi. Niachie hayo nitasuluhisha,” baba mkwe alimtuliza mwanadada.

Inasemekana kuwa, jamaa alipigiwa simu na baba yake na kufahamishwa aende nyumbani haraka iwezekanavyo kushughulikia  jambo la dharura.

Alipofika nyumbani hakuamini alipogundua kwamba lililokuwa la dharura ni takwa la mkewe.

“Baba mimi huwezi kunilazimisha kumbeba mke hadi mjini, gharama itakuwa juu sana,”  jamaa alijaribu kujitetea.

Hata hivyo wazazi wake hawakumpa nafasi mbali walimwambia ikiwa hangeenda na mkewe  mjini, amtaliki mara moja.

“Mimi sina haja na mke mwingine, nilitosheka na mama yako. Kama huendi na huyo wako, mrudishie wazazi wake mara moja na ujue kwamba hutaoa mwingine umlete hapa,” jamaa alionywa vikali na baba yake.

Kulingana na mdokezi, jamaa hakuwa na budi ila kurudi na mkewe mjini ingawa shingo upande.

Share Bookmark Print

Rating