Jombi alishwa mijeledi na chifu kwa kumbeza

Imepakiwa Friday January 29 2016 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Kalameni aliyejidai jasiri zaidi alijipata pabaya baada ya kumtusi chifu wa eneo hili.

NYASERO, NYAMIRA

KALAMENI aliyejidai jasiri zaidi alijipata pabaya baada ya kumtusi chifu wa eneo hili.

Inasemekana kuwa polo alianza kumtusi chifu alipomuita ofisini baada ya kupata malalamishi  kutoka kwa wakazi kwamba alikuwa 'akiwaharibu’ wasichana wao.

“Nimekuita hapa ili unieleze ikiwa madai niliyoyasikia kukuhusu ni ya kweli,” chifu alimueleza polo.

Hata hivyo, polo hakushtushwa na maneno ya chifu.

Inasemekana kuwa baada ya chifu kumfafanulia madai yote, polo alianza kupandwa na hasira.

What is the problem with that? Mlitaka nimtafute wapi mchumba? Hata mwenye kuleta kesi kama hiyo kwako hana aibu hata kidogo. Kwani alitaka kumuoa msichana wake?” polo alimuuliza chifu kwa hasira.

“Kwanza si huyo pekee yake. Kuna wengine wawili ambao walileta malalamishi kama hayo tu. Wote wanadai kuwa wewe unawaharibu wasichana wao ilhali wangali wanasoma,” chifu alimueleza polo.

“Kwani hauna kesi nyingine ya kusikiza? Tafuta kesi kubwa ya kusikiza. Jina lako ni kubwa sana kuliko hii kesi yangu. Acha aibu ndogondogo bwana chifu. Kama huna kazi nitakutafutia,” jamaa alimueleza chifu.

Inasemekana kuwa chifu pia alipandwa na hasira na kuanza kumzomea polo ila polo akamzima.

“Wewe ni mjinga sana. Hayo madai si ya kuniita hapa,” polo alimzomea chifu huku akiondoka.

“Sasa umeamua kunitusi? Unanidharau sasa? Basi tuone nani ataumia!” chifu alifoka.

Kulingana na mdokezi wetu, chifu aliwaita polisi tawala wake. “Nao polisi walifika kwa haraka sana ambapo walimpata polo akiwa bado anamrushia chifu cheche za matusi. Polisi walimweka pingu na kumuelekeza kituoni,” alisimulia mdokezi.

Inasemekana polo alipewa viboko visivyohesabika. “Aliapa kutorudia makosa hayo,” alieleza mdokezi.

Share Bookmark Print

Rating