Binti azomewa na kina mama kwa kutovaa sidiria

Imepakiwa Monday February 1 2016 | Na GRACE KARANJA

Kwa Muhtasari:

Demu mmoja mtaani hapa alijipata pabaya, akina mama walipomuaibisha mbele ya umma wakidai alikuwa na mazoea ya kutovalia sidiria.

DANDORA, NAIROBI

DEMU mmoja mtaani hapa alijipata pabaya, akina mama walipomuaibisha mbele ya umma wakidai alikuwa na mazoea ya kutovalia sidiria.

Yasemekana haikuwa mara ya kwanza akina mama hao kumuonya binti huyo dhidi ya kutovaa vizuri lakini hakutilia maanani onyo hilo.

Walisema tabia ya mwanadada huyo ilikuwa ikiwaaibisha wanawake na hawangekubali kudharauliwa na wanaume. Baadhi walisema kipusa huyo alikuwa na nia mbaya.

Asubuhi ya kisanga, demu alienda dukani alipokutana na akina mama wawili waliomlazimisha kurudi kwake kuvalia sidiria lakini akawadharau akisema mavazi yake hayakuwahusu.

“Mimi nikikosa kuvalia sidiria inawahusu nini, haya ni maisha yangu, niacheni niishi ninavyotaka,” demu aliwajibu kwa dharau akina mama.

Majibu hayo yaliwakera sana akina mama hao na wakamgeukia demu kana kwamba walitaka kumvua nguo wamwache uchi.

“Kama hutaki kuvalia vizuri itakubidi uhame hapa kama sivyo wacha tukuvue hii nguo ya juu utembee hivyo watu wakuone vizuri,” akina mama waliojawa na ghadhabu walimwambia demu. Hata hivyo, mwanadada huyo hakushtushwa na vitisho vyao.

Kulingana na mdokezi masaibu ya demu yalizidi  akina mama wengine walipofika na kuelezwa kilichokuwa kikiendelea na wakawaunga  mkono wenzao wakimwambia demu kwamba ni kwa manufaa yake kuvaa vizuri.

Hata hivyo, walipinga hatua ya kutaka  kumvua nguo mwanadada huyo wakisema ni tendo la uhalifu na wanaweza kushtakiwa kwa kufanya hivyo.

“Heri tumuache kwa sasa kisha akubali kuacha  shughuli zake arudi akavalie sidiria. Sio vizuri kumvua mtu nguo. Mnaweza kufungwa jela kwa kufanya hivyo,” alisema mama aliyemwonea huruma demu huyo.

Kulingana na mdokezi, demu alitimka mbio asionekane tena eneo hilo la kisanga.

Share Bookmark Print

Rating