Demu amchemkia polo kwa kumtongoza hadharani

Imepakiwa Tuesday February 2 2016 | Na TOBBIE WEKESA

Kwa Muhtasari:

Umachachari wa polo wa hapa ulimtia mashakani alipozomewa na kidosho kwa kufanyia mzaha maumbile yake ya kuvutia.

SIREMBE, SIAYA.

UMACHACHARI wa polo wa hapa ulimtia mashakani alipozomewa na kidosho kwa kufanyia mzaha maumbile yake ya kuvutia.

Kulingana na mdokezi, kipusa huyu alipita mbele ya mapolo wanne ambapo mmoja alivutiwa na maumbile yake.

“Madamu, si huyu amenimaliza na hizo 'fundamentals’ zake. Beib, can I escort you please?” polo  alimuuliza kidosho. Inasemekana kipusa alisimama na kumuangalia polo.

“Unaweza kurudia uliyotamka sasa hivi,” kipusa alimuuliza polo kwa ukali.

“Enyewe uko chonjo tu sana. Nataka tu kuandamana na wewe,” polo alimueleza kipusa huku wenzake wakicheka .

“Ni mimi unaita fundamentals?” kipusa alimuuliza polo naye jamaa akaendelea kumjibu.

“Madam usikasirike. Kusema kweli umezibeba poa,” polo alimueleza kidosho.

Jibu hilo lilimfanya  kidosho kupandwa na hasira na kuanza kumzomea polo.

“Wewe ni mjinga sana. Umeamua kuja hapa kuwapa watu majina?  You must be a very big idler. Mshenzi wewe,” kipusa alimzomea polo. Kulingana na mdokezi, polo alinyamaza kwa sababu kipusa hakumpa ruhusa ya kuongea tena.

“Watu walianza kukusanyika eneo la tukio hili kila mmoja akitaka kujua kilichokuwa kikiendelea,” alieleza mdokezi.

“Angalieni huyu mjinga. Mimi nilikuwa nikipita kisha akaanza kuniita fundamentals. I don’t like that nonsense,” kipusa alieleza umati.

Kwa mujibu wa mdokezi, kipusa aliamua kumpa polo onyo kali sana. “Wewe sikia kuanzia leo, nikisikia tena ukilitamka hilo neno, utajua kilichomnyoa kanga manyoya shingoni,” kidosho alimueleza polo.

Inasemekana kuwa polo na wenzake waliamua pia kutoweka. “Wewe endelea kupayuka. Ukimaliza au ukichoka, nenda kwenu,” polo alimueleza kipusa huku akienda.

“Kipusa naye aliamua kuendelea na safari yake.” alieleza mdokezi.                  

Share Bookmark Print

Rating