Agutushwa na makofi ya mkewe kwa kulowesha kitanda

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, February 2  2016 at  15:23

Kwa Muhtasari

Kalameni wa hapa anajuta baada ya kupokezwa kichapo kikali na mkewe kwa kwenda haja ndogo kitandani.

 

MUGOIRI, MURANGA

KALAMENI wa hapa anajuta baada ya kupokezwa kichapo kikali na mkewe kwa kwenda haja ndogo kitandani.

Yasemekana polo huwa na vituko anapolewa kiasi cha kukojoa kitandani. “Jamaa anapolewa, huwa hawezi  kuzuia mkojo wake,” alisema mdokezi.

Minong’ono inaarifu kwamba mkewe hulazimika kufua malazi ambayo jamaa hulowesha.

“Kila wakati kalameni akipitia kwa mama pima, huenda haja ndogo kitandani na akiulizwa na mkewe huwa mkali,” alisimulia mdokezi. Siku ya kioja yasemekana kalameni alishinda  kwa mama pima.

Alifika kwake mwendo wa saa nne za usiku akiwa chakari. Baada ya chakula, alijilaza kitandani na kuzama kwenye usingizi.

Mwendo wa saa nane za usiku  aligutushwa na makofi mazito aliyoangushiwa na mkewe alipogundua  alikuwa amelowesha kitanda kwa mkojo.

“Wewe umekuwa mtoto wa kukojoa kitandani ovyo ovyo? Una tofauti gani na  watoto jamani? Huna hata aibu ukikojoa kitandani mzee mzima kama wewe!

Leo utanitambua na kamwe sitavumilia tabia kama hii,” alichemka mama huyo akimuangushia kichapo kikali.

Kulingana na mdokezi, wiki mbili sasa zimepita buda hajaonekana kwa mama pima tena.

Yasemekana kwamba huwa anaonekana akishughulika shambani na kutunza mifugo wake.