Pasta na polo vitani waking'ang'ania mjane

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, February 11  2016 at  12:34

Kwa Muhtasari

Sinema ya bure ilishuhudiwa kwenye boma moja mtaani hapa pasta na kapera walipolishana makonde waking’ang’ania mjane.

 

GATUNG’ANG’A, Nyeri

SINEMA ya bure ilishuhudiwa kwenye boma moja mtaani hapa pasta na kapera walipolishana makonde waking’ang’ania mjane.

Mama huyo ni mshirika wa kanisa analohudumu pasta huyo na yasemekana tangu afiwe na mumewe miezi sita iliyopita, mhubiri huyo alikuwa akimtembelea mara kwa mara.

Duru zinaarifu kwamba kapera huyo pia alikuwa akipiga kambi kwa mama huyo. “Wote walikuwa na lengo la kumnasa mjane huyo na kuanza uhusiano wa kimapenzi” alisema mdokezi.

Minong’ono inaarifu pasta alikuwa akimtembelea jamaa akidai alitaka kumfariji. “Barobaro naye alikuwa akipata pasta akimhubiria mjane japo hakudhani alikuwa akimmezea mate,” alieleza mdokezi.

Inasemekana siku ya kioja pasta alimtembelea mama huyo jioni na akaandaliwa chakula. Baada ya chakula, wawili hao walizama katika mahaba kwenye kochi sebuleni.

Hawakujua kuwa kapera angefika kwa mjane huyo siku hiyo.

Jamaa alipigwa na butwaa kupata pasta  akimpokeza mabusu moto moto. Kwa hasira, alimporomoshea pasta mangumi na mateke.

“Haya ndiyo mahubiri ambayo huwa unayaleta hapa? Huwezi tulia kwa mkeo? Huyu mama achana naye, tena kaa mbali kabisa, yeye ni mali yangu. Nimemsimamia tangu afiwe na mumewe,” alichemka kapera.

“Hei, koma hapo, nani alikueleza pasta hana hisia za mapenzi? Nimekuwa nikimlisha chakula cha kiroho na sasa anahitaji cha mwili,” alifoka pasta.

Yasemekana mama huyo alipiga kamsa zilizoalika watu wakaenda kuwatenganisha.

Walioshuhudia kisanga hicho waliachwa midomo wazi na baadhi wakaangua kicheko. Wawili hao walifurushwa kwa mama huyo na haikujulikana ikiwa walirudi kwake tena.