Weita atiwa adabu kwa kuwapora walevi

Na CORNELIU MUTISYA

Imepakiwa - Thursday, February 11  2016 at  12:51

Kwa Muhtasari

Mhudumu wa baa katika soko hili aliamua kumkubali Yesu kuwa mwokozi wa maisha yake alipopokezwa kichapo na walevi walipogundua hila yake ya kuwaongezea bili kila wakati wakilewa chakari.

 

KITHUNGUNI, MACHAKOS

MHUDUMU wa baa katika soko hili aliamua kumkubali Yesu kuwa mwokozi wa maisha yake alipopokezwa kichapo na walevi walipogundua hila yake ya kuwaongezea bili kila wakati wakilewa chakari.

Kulingana na mdokezi, kipusa huyo alizoea kuwaongezea walevi bili ya pombe akinuia kuwalaghai hela.  Hakuogopa kuchomoa pesa kutoka kwa mifuko ya wateja wake wakilewa chopi.

“Alizoea kuwatapeli walevi hela zao. Kwa kuwa tabia ni mazoea, aliendelea kuwalaghai makastoma hadi wakapungua,’’ akasema mdokezi.

Inasemekana kwamba, sifa zake mbovu  zilizagaa kote na walevi wakapanga njama ya kumkomesha. Waliamua kujivinjari katika baa hiyo na wakamrai mmoja wao aanze kusinzia akijifanya amelewa chakari.

Duru zaarifu kipusa huyo alipoona jamaa alikuwa akisinzia, alimpelekea risiti aliyoongezea Sh 1,000 juu ya bili yake.

Walevi walikasirika na wakampokeza kichapo kabla ya kuokolewa na mwenye baa aliyefika mara moja aliposikia kelele.

Kufuatia kisa hicho, mwanadada huyo aliacha kazi ya kuuza baa na akaokoka. Kwa wakati huu, yeye ni mwanakwaya shupavu katika kanisa moja la kiroho eneo hili na kiongozi wa kikundi cha wanarika.