Polo aangushiwa kichapo kwa kukiri alimramba maiti

Imepakiwa Sunday February 14 2016 | Na SAMMY WAWERU

Kwa Muhtasari:

Kioja kilitokea katika ibada moja ya mazishi mtaani hapa jamaa alipoangushiwa kichapo kikali kwa kufichua kwamba marehemu alikuwa mpango wake wa kando licha ya kuwa mke wa mtu.

NDUNYU NJERU, Nyandarua

KIOJA kilitokea katika ibada moja ya mazishi mtaani hapa jamaa alipoangushiwa kichapo kikali kwa kufichua kwamba marehemu alikuwa mpango wake wa kando licha ya kuwa mke wa mtu.

Yasemekana jombi alikuwa rafiki wa karibu wa mume wa mama aliyefariki.

“Mume wa marehemu alishangaa kugundua rafiki yake alikuwa akichovya asali yake,” akasema mdokezi.

“Wakati  mume wa marehemu alipokuwa akipigwa picha karibu na jeneza la marehemu mkewe, kalameni alitokea na kujiunga naye akisema ilikuwa hatua ya kumfariji,” alisimulia mdokezi.  Kitendo chake hicho kilishtua waombolezaji kwa sababu hakikuwa cha kawaida.

Wakati wa kutoa rambirambi, kwa jamaa na marafiki, polo aliomba nafasi.

“Nina huzuni mwingi kwa kumpoteza marehemu aliyelala hapa. Jamaa zake mpokee pole zangu. Kwa kweli hakuwa rafiki tu, bali alikuwa mpango wangu wa kando.

Naomba radhi kwa mumewe, ninafahamu hakujua uhusiano uliokuwepo kati yetu,” alisema polo.

Kalameni alipoweka maikrofoni chini, mume wa marehemu alimrukia na kumkaba koo huku  akimuangushia mangumi na mateke.

“Leo utanieleza sababu ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wangu,” mume wa marehemu alichemka.  Kwa dakika kadhaa, ibada ya mazishi iligeuka kuwa uwanja wa vita polo akicharazwa.

Kalameni aliokolewa na pasta aliyeongoza ibada hiyo na waombolezaji waliomsihi mumewe kumsamehe.

“Neno la Mungu kwenye Biblia linasema tusamehe mara saba kwa sabini na jua lisitue kabla hatujasamehe waliotukosea ili tuweze kuurithi ufalme wa Mungu” alisema pasta huyo.

Kizaazaa hicho kilitulia na ibada akaendelea polo akishauriwa kuheshimu ndoa za watu.

Share Bookmark Print

Rating