Uganga wazua ngumi kati ya wake-wenza

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Monday, February 15  2016 at  12:48

Kwa Muhtasari

WAKAZI wa eneo hili walitazama sinema ya bure pale wake-wenza walipochapana makonde mmoja alipomlaumu mwenzake kwa kwenda kwa mganga kumzuia mume wao kutembelea  boma lake.

 

NAITIRI, BUNGOMA

Kulingana na mdokezi, mke wa kwanza alimvamia na mke wa pili na kuzua rabsha.

“Njama yako nimeijua. Unawezaje kwenda kwa mganga kumzuia baba ya watoto wangu kuja kwangu? Chunga unacheza na simba. Uliolewa hili boma juzi halafu unaanza kuleta ujuaji,” mke alimfokea mwenzake.

“Najua nilikuja hili boma juzi lakini lazima ujue kuwa kila mtu ana kwake.

Nani alikuambia mimi nilienda kwa mganga?  Haikosi hujui kumtunza mzee na ndio maana hataki kuja kwako,” mke wa pili alimjibu mwenzake.

Malumbano yaliendelea kwa muda.

“Nani alikuambia mimi sijui kumtunza  mume? Wewe ukija hapa,  nilikuwa nimeishi na yeye miaka gapi? Baada ya kukuhurumia na nikakubali uwe mke mwenzangu, unaanza kuniendea kwa mganga? Leo utanijua,”  mke wa kwanza alimuambia mwenzake huku akimrukia.

Penyenye zinasema  kabla ya wanawake hawa kuumizana, mume wao alifika.

“Shida yenu ni ipi? Mbona mwaniletea aibu?” jamaa aliwauliza. 

“Baba boi kabla hiki kinyangarika kuja hapa, tulikuwa tumeishi nawe miaka migapi?” mke wa kwanza alimuuliza mumewe.

“Iweje leo  anaenda kwa mganga ili kukuzuia wewe kuja kwangu? Lazima sasa aniondokee,”pili alimuambia mumewe huku akimzaba mwenzake makofi.

Inasemekana jamaa alishindwa kutatua mgogoro huo. “Ilibidi atoweke majirani walipoanza kukusanyika kwa wingi,” alieleza mdokezi.

Kulingana na mdokezi wetu, iliwabidi majirani kuingilia kati ili kuwatenganisha wanawake hao. Baadaye kila mtu alienda zake huku wakitafakari vituko vya wake wenza hao.