Pasta alimwa makonde kwa kurushia mistari kisura wa muumini

Imepakiwa Monday February 29 2016 | Na SAMMY WAWERU

Kwa Muhtasari:

MHUBIRI wa kanisa moja mtaani hapa, nusra ajikatie tikiti ya bure ya kwenda jongomeo alipofumaniwa kwa kidosho na mpenzi wa mwanadada huyo.

MAKUTANO, Mwea

Kipusa huyo ni mfuasi wa kanisa la pasta huyo. Yasemekana pasta huyu alikuwa akimezea mate kisura huyo na kila wakati alikuwa akizuru kwake kwa madai ya kumuombea.

“Siku mbili hazingepita kabla pasta huyo kwenda kwa kipusa huyo akisingizia alikuwa akilisha kondoo wake chakula cha kiroho” akasimulia mdokezi.

Licha ya mwanadada kumfahamisha alikuwa na mpenzi aliyetarajia kufunga pingu za maisha naye, pasta alitia masikio pamba  na akaendelea kumtembelea kumrushia mistari ya mapenzi.

Yasemekana siku ya kioja, mhubiri huyo aliaga mkewe akimweleza alienda kutembelea waumini kondoo wake waliohitaji maombi.

Ulikuwa mwendo wa saa mbili za jioni akiwa kwa kipusa na baada ya kuandaliwa chakula, pasta alikariri mistari kadhaa ya Biblia kisha akafichua kilichompeleka kwa kipusa.

“Dada katika Yesu, mimi ni binadamu kama wale wengine. Zaidi ya yote mimi ni mwanamume aliye na hisia za mapenzi na kusema ukweli ninakupenda,” alisema mhubiri huyo na kuanza kumpapasa mwanadada huyo.

Mlango haukuwa umefungwa na mpenzi wa kipusa aliyemtembelea  aliingia bila kubisha na kumfumania  pasta akinyemelea asali yake. 

“Huku ndiko kulisha kondoo wako chakula cha uzima? Huyu ni mke wangu mtarajiwa na uniskie vizuri! Huna hata aibu ukiacha mkeo, pasta mzima kutafuta mpango wa kando,” alichemka polo akimcharaza mtu wa Mungu.

Mhubiri huyo alilazimika kuchana mbuga akiwa na Biblia yake mkononi kuepuka aibu. Inasemekana habari hizo zilimfikia mkewe na wafuasi wake kanisani na haijulikani hatua aliyochukuliwa baadaye.

Share Bookmark Print

Rating