Utingo mdaganyifu akutana na saizi yake

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Monday, March 28  2016 at  12:01

Kwa Muhtasari

DANDORA, Nairobi

UTINGO mmoja alijipata pabaya baada ya kukabwa koo na abiria wa kike aliyekasirika baada ya kugundua kwamba alimdanganya.

 

Kulingana na mdokezi wetu, kabla ya abiria huyo kupanda gari, makanga alimuarifu lingepitia eneo alilotaka kushukia. “Kipusa alishawishika na kuliabiri gari,” alieleza mdokezi.


Inasemekana kuwa njiani, utingo alianza kuchukua nauli kutoka kwa abiria. Ghafla gari lilipiga kona kuelekea sehemu tofauti na alikokuwa akienda kipusa.


“Sasa unanipeleka wapi?” kipusa alimuuliza utingo.


Kulingana na mdokezi, kipusa alipandwa na hasira. “Look at this idiot. Wakati nilipanda hili gari uliniambia nini? Leta pesa zangu hapa haraka,” kipusa alimueleza utingo.


“Kiendacho kwa mganga hakirudi. Kama unataka basi shuka,” utingo alimueleza mwanadada kwa dharau.


Ugomvi baina ya utingo na kipusa uliendelea kushika kasi kipusa akisisitiza kuwa ni lazima arejeshewe nauli yake. 
Inasemekana kuwa gari lilipofika kwenye steji lilisimama ili kuwachukua wateja wengine.


“Kipusa alishuka huku akimvuta polo shati. “Nilikwambia ninaenda wapi? Na hapa ni wapi? Mbona mnapenda kukaa vichwa ngumu hivyo? Leo utajua ya kwamba hata sisi tumezaliwa,” kipusa alimkaripia utingo.


Inasemekana kuwa iliwabidi madereva na makanga wengine kuingilia kati ili kumuokoa jamaa. “Alipopata mwanya wa kutoroka, polo alichomoka mbio bila kuangalia nyuma. Alipomuona utingo akila mbio, naye kipusa aliamua kumfuata unyounyo,” alieleza mdokezi.


Kulingana na mdokezi, watu walishangazwa na mbio ya polo.

“Kama huyu mwanadada anatishia huyu mwanamume, je, ingekuwa vipi kama ni mwanamume aliyekuwa akilalamika? Si mambo yangekuwa mengine,” mzee mmoja ambaye alikuwa katika sehemu ya tukio hili alisema.