Aibu kwa mzee wa kanisa baada ya kufichuka alizaa na kiruka njia

Na OSCAR KAKAI

Imepakiwa - Sunday, April 3  2016 at  13:11

Kwa Muhtasari

KAPENGURIA MJINI

KIOJA kilizuka katika kanisa moja mjini hapa mzee wa kanisa alipotupiwa mtoto na mpango wake wa kando ibada ikiendelea.

 

Kisanga hiki kilitendeka mama alipofika kanisani kwa  nia  ya kumuaibisha mzee huyo.

Duru ziliarifu kuwa buda huyo alikuwa amekataa kumsaidia kumtunza mtoto huyo.

Yasemekena kuwa jamaa alikuwa akihepa majukumu kama baba ya mtoto aliyekuwa na umri wa mwaka  mmoja.

Buda huyo alikuwa ameificha familia yake kuhusu suala hilo na ni watu wachache walikuwa wanaelewa.

Mama alienda moja kwa moja alikoketi mzee huyo pasta alipokuwa akihubiri.

“Leo ni leo lazima kanisa lijue mambo ambayo huwa unajificha. Huwezi kuzaa mtoto kisha ukose kulea,”alisema mama aliyejawa na ghadhabu.

Baada ya kukosa msaada kutoka kwa wahudumu wa kanisa hilo, mama aliamua kumrushia mzee mtoto huyo.

Ibada  ilisimamishwa kwa muda huku walinzi wa kanisa hilo wakifika kwa haraka ili kumuokoa mzee huyo.

Ilibidi  walinzi hao kumfurusha mama na mtoto haraka.

Mzee huyo alibaki kimya kwenye kiti huku akijifanya  alikuwa amezama katika maombi.

Kisanga hiki kiliwaacha waumini  vinywa wazi kwa sababu buda huyo ni mmoja wa viongozi wakuu katika kanisa hilo.

Mdaku wetu alituarifu kwamba mama alikuwa amemweleza mke  wa mzee huyo ajiandae kwa  kisanga.

“Mke wa kiongozi huyo ambaye alikuwa kwenye kanisa hilo alitulia na kushindwa la kufanya,” akasema mdokezi.

Ilibidi wazee wa kanisa hilo kuingilia kati na kumueleza mama kuwa watamueleza mzee aweze kuwajibika.

“Mama tulia tutamueleza mzee aweze kutoa msaada kwa mtoto,”mzee mmoja alisikika akisema.

Baada ya kuambiwa hayo, mama aliondoka akiapa kumuonyesha mzee cha mtema kuni.