Polo mtanashati afanya demu na mdosi wapigane

Na CORNELIUS MUTISYA

Imepakiwa - Monday, April 4  2016 at  09:59

Kwa Muhtasari

KIOJA kilishuhudiwa mjini hapa demu alipotwangana na mke wa mwajiri wake waking’ang’ania barobaro aliyekuwa mteja katika hoteli waliyokuwa wakichapa kazi.

 

Kulingana na mdokezi, mke wa bosi alikuwa keshia katika hoteli ya mumewe huku demu akiwa weita.


Huduma yao mufti ilifanya hoteli hiyo kuvuma mno na kupendwa na makastoma wengi.


“Makastoma walifurika katika hoteli hiyo kwa sababu ya mapishi kibao na huduma ya hali ya juu,’’ akasema mdokezi.


Penyenye zaarifu kwamba, miongoni mwa wateja hao alikuwa barobaro mmoja aliyefanya kazi ya kuuza bima.

Utanashati na upole wake ziliwafanya mama na demu huyo kumtamani japo kwa siri.


Inasemekana kwamba, demu alichota fikira za barobaro huyo na wakawa wapenzi wa chanda na pete. Hata hivyo, mama huyo alipogundua kuwa jitihada zake za kumzuzua barobaro huyo zilikuwa zimegonga mwamba, alikasirika.


Siku ya kisanga, barobaro huyo alifika hotelini mwendo wa saa sita adhuhuri kwa chakula cha mchana. Alikaribishwa kwa furaha na bashasha na demu huyo na wakapiga gumzo kwa dakika kadhaa kabla ya kuagiza maankuli. Mama alikuwa akiwatazama akikereka.


Inasemekana mama alianza kumzomea demu huyo huku akimwambia akomeshe tabia ya kuwasumbua wateja wake. Vurugu zilizuka baina yao nusura wachafuane sura.


“Mama alimzomea demu akimwambia hakuwa na ruhusa ya kuingilia wateja wake,’’ alisema mdokezi.


Kulingana na mdokezi, maji yalizidi unga mwanadada alipomfokea mama huyo na kumwambia alikuwa amezeeka.

na alipasa kuwaachia uwanja na vita vikaanza.


Ilibidi wateja kuingilia kati na kuwatenganisha na kuwashauri haikuwa jambo la busara kuzozana mbele ya makastoma.