Mke arukia kalameni kula kwa demu jirani

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Sunday, April 17  2016 at  14:15

Kwa Muhtasari

TENKWEN, Bomet

KALAMENI wa eneo hili alipata aibu ya mwaka alipozomewa na mkewe baada ya kupatikana akila ugali katika nyumba ya kipusa jirani yao.

 

Inasemekana kuwa mke wa polo alikuwa akitoka sokoni kuuza mahindi, alipomuona mumewe katika nyumba ya kipusa huyo.


Kulingana na mdokezi wetu, mume wa kipusa alikuwa jijini anakofanya kazi na fununu za mtaa zilidai polo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kipusa huyo.

Inasemekana kuwa polo alijaribu kujificha nyuma ya mlango lakini mkewe alikuwa amemtambua kutokana na mavazi yake. “Nimeona mtu hapa kama bwanangu. Kwani ameingia wapi?” mama alimuuliza kipusa. “Ni kama wewe umeona shetani. Bwanako hayuko hapa,” alijibu kipusa.


Duru zinasema kuwa mke wa polo aliamua kuingia ndani ya nyumba ya kipusa na akampata jamaa. “Na huyu ni nani? Nilikuona ukila chakula hapa. Huna aibu hata kidogo,” mama alianza kumzomea polo.

Njaa
“Ni mara ngapi nimekuuliza kuhusu uhusiano wako na huyu mwanamke kisha unapinga?” mama aliendelea kumuuliza polo. “Mimi nilikuwa na njaa. Singekungoja urudi kutoka sokoni ndio unipikie. Niliona ni afadhali nije nile hapa,” polo alimjibu mkewe.


Kulingana na walioshuhudia kisa hiki, mama alianza kumzomea polo bila kuogopa chochote. “Nani hajui mambo yako na huyu bibi? Unajifanya hapa eti una njaa. Kile chakula nilikupikia kwani umemaliza? Mimi najua huyu ni mpango wako wa kando.”


Inasemekana kuwa watu walianza kufurika eneo hilo. “Kila mtu alishangazwa na maneno ya mke wa polo,” alieleza mdokezi. Polo alishindwa kumkabili mkewe. “Sitaki kukuona tena,” mkewe alisema huku akiondoka.