Polo alimwa na mke kwa kukataa kutoa namba siri ya ATM

Imepakiwa - Sunday, April 17  2016 at  14:20

Kwa Muhtasari

DANDORA, Nairobi

JOMBI wa mtaa huu alijipata pabaya baada ya mkewe kumkabili bila huruma na kumjeruhi alipokataa kumpa nambari ya siri ya ATM yake.

 

Kulingana na penyenye, haikuwa mara ya kwanza ya jombi kuonekana akinuna mwisho wa mwezi ila hakuna aliyejua masaibu aliyokuwa akipitia.


Inasemekana kwamba jamaa alirejea nyumbani kutoka kazini akiwa amelewa.


Hapo ndipo ugomvi kati yake na mumewe ulipoanza mkewe akitaka pesa za matumizi.


“Wewe ni gwiji wa kulewa tu lakini hukumbuki kwamba tunahitaji chakula. Si kwanza ungeniletea pesa kisha uende kujiunga na walevi wenzako. Nipe ATM na nambari ya siri sasa hivi,” mkewe aliteta.


Ni katika mabishano yao ambapo mama alimpiga mumewe lakini kwa bahati, jirani mmoja alimsikia jamaa huyo akimwambia mkewe kwamba hangempa nambari hiyo.


“Yaani wewe unaweza kuniumiza kwa sababu ya pesa zangu, wacha nikuambie, hata ukitaka kuniua, niue tu lakini nambari ya siri ya kadi yangu sikupi,” jamaa alimwambia mkewe.


Kulingana na mdokezi, jirani alimlazimisha mke wa jamaa kuufungua mlango na alipokataa aliwaita majirani wengine na wakugundua kwamba alikuwa amempiga mumewe na kumjeruhi.