Mbwa wararua polo akinyemelea demu

Imepakiwa Tuesday April 26 2016 | Na KIMANI wa NJUGUNA

Kwa Muhtasari:

NKUBU, Meru

POLO wa hapa alipata majeraha aliposhambuliwa na mbwa wakali akimsubiri kipusa aliyekuwa akimmezea mate.

Penyenye zinasema jamaa huyo anajulikana kwa tabia yake kuwaandama vipusa kila wakati. Hivi majuzi, alikutana na mwanadada wakiwa kwenye mkutano wa kanisa.


“Wawili hao walianza uhusiano wa kimahaba na ikawa ni kawaida yao kukutana kila Jumamosi ili wale 'tende’ pamoja,” akasema mdokezi.


Inasemekana mama wa mwanadada huyo huwa anahudhuria mkutano wa akina mama kila Jumamosi jioni. Lakini naye baba wa demu huyo huwa anajiunga na marafiki vilabuni kuburudika hadi usiku na akirudi nyumbani mbwa wake wakali huwa wanafunguliwa.


Mambo yalienda mrama Jumamosi iliyopita kwani buda hakuhudhuria kikao cha wazee na kumfanya mkewe kuwa nyumbani kinyume na desturi, ili amshughulikie mumewe.


Kwa sababu ambazo hazikubainika, kidosho hakuwasiliana na jamaa ili wabadilishe mpango wao.


Isitoshe, mbwa wa boma walifunguliwa mapema kwa sababu mzee hakutoka nyumbani. Ilipofika saa mbili jioni, polo alielekea katika boma la mpenzi wake kama ilivyokuwa desturi na kusimama karibu na dirisha la chumba cha kidosho ambapo alibisha.


Kabla ya dakika kupita, mbwa walitokea na kuanza kumshambulia jamaa. Kilio cha polo kiliwavutia wote waliokuwa katika boma hilo.


“Wuuii! Wuuuii! Wuuuui! Mimi si mwizi! Mimi ni shemeji yenu,” akalia jamaa katika juhudi za kujiokoa.


Ilibidi kidosho kuingilia kati na kumnusuru polo huyo dhidi ya kutafunwa na mbwa na kukiri kwamba alikuwa mpenzi wake.


Hapo ndipo wazazi wake kidosho huyo walipomuonya polo na kuapa kumpatia funzo ambalo hatawahi kusahau maishani akirudia tabia hiyo.

Share Bookmark Print

Rating