Demu alishwa kipigo baada ya kufumaniwa na mpango wa kando

Imepakiwa - Friday, May 6  2016 at  10:45

Kwa Muhtasari

DALAS, Embu

Mwanadada kutoka eneo hili alijipata pabaya mumewe alipompokeza kichapo na kumtema baada ya kumfumania katika hali ya kutatanisha na buda aliyeshuku kuwa mpango wake wa kando.

 

MWANADADA kutoka eneo hili alijipata pabaya mumewe alipompokeza kichapo na kumtema baada ya kumfumania katika hali ya kutatanisha na buda aliyeshuku kuwa mpango wake wa kando.


Penyenye zilizotufikia zasema kwamba mwanadada huyo alikuwa akija nyumbani na pesa nyingi licha ya kutofanya kazi.
“Maisha yake yalibadilika akawa na pesa nyingi licha ya kutofanya kazi,” akasema mdokezi.


Inasemekana kuwa mumewe alipomuuliza alikotoa pesa hizo za kununua vipodozi kila wakati alimwambia kwamba wanaume ni wengi walio na mali.


“Mkewe alimjibu kwa dharau na kumwambia kwamba wanaume ni wengi ambao wana pesa na hawana haja nazo,” alisema mdokezi.


Siku ya kioja, mumewe mama alijipodoa na mumewe akamuuliza alikokuwa akienda, naye akamdanganya kwamba alikuwa akipeleka mchango katika kikundi cha akina mama.


“Kama ni lazima ufahamu ninakoenda kila wakati, leo ni siku ya chama, ninapeleka hela za akina mama,” alijibu.
Ni katika baa moja iliyoko eneo hili alipomfumania mkewe na buda mmoja wakipigana mabusu.


“Shika hizi hela ukanunue kile unachohitaji kwa sasa, kisha mwisho wa mwezi nitakupa zile nilizokuahidi. Kumbuka kuwa mjanja mumeo asijue uhusiano wetu na wewe,” buda alimweleza mwanadada.


Mumewe hakungoja tena, alijitokeza na kuanza kumchapa mkewe.


“Wewe hata hujiheshimu, unajiuza kwa mzee kama huyu rika la baba yako kwa sababu ya pesa,” jamaa alichemka kwa hasira na kuchukua hela alizoficha kwa sidiria na kuzitupa.


Jamaa huyo alisikika akimweleza mkewe kumfuata buda aliyeponyoka na kuingia kwa gari na kutoroka.