Demu aanika wazi ufisi wa polo kwa harusi

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Sunday, May 15  2016 at  13:53

Kwa Muhtasari

NDAUNI, Makueni

Kizaazaa kilizuka katika kanisa moja eneo hili kipusa alipomtaka pasta kusimamisha harusi akidai alikuwa na mimba ya bwana harusi.

 

KIZAAZAA kilizuka katika kanisa moja eneo hili kipusa alipomtaka pasta kusimamisha harusi akidai alikuwa na mimba ya bwana harusi.


Kulingana na mdokezi, kipusa aliingia kanisani na kuelekea moja kwa moja hadi kwenye altari. “Wewe akili yako inafanya kweli? Kwa nini unapenda kuchezea mademu?” kipusa alimuuliza polo.

Inasemekana kuwa waumini kanisani walisimama wote kujionea yakiendelea. “Nimeuliza unafanya nini hapa?” kipusa alizidi kumuuliza polo.


Penyenye zinasema kuwa polo alikuwa amepanga harusi hiyo kwa siri bila hata kuwaeleza baadhi ya marafiki zake.
Kulingana na mdokezi, pasta alisimama na kujaribu kumshawishi kipusa kutulia.

“Wewe pia achana na mimi kabisa. I’m carrying his child. Na leo ananifanyia haya,” kipusa alimueleza pasta. Inasemekana kuwa pasta alipigwa na butwaa aliposikia maneno ya kipusa. “Una uhakika na yale unayosema?” pasta alimuuliza kipusa.


Duru zinasema kuwa kila mtu kanisani alianza kucheka. “Huyu jamaa alikuwa ameahidi kunioa. Hata tulikuwa tumepanga kwenda kujitambulisha kwa wazazi. Leo ananifanyia haya. Huyu ni mtu wa aina gani?” kipusa alimuuliza pasta.


Inasemekana kuwa polo alimweleza pasta aliachana na kipusa yule. “Pasta achana naye. Nilimtema kitambo. Mchumba wangu kwa sasa ndiye huyu. Kama ana mimba yangu mimi sijui. Wewe endelea na harusi,” polo alimueleza pasta.


Kwa hasira, kipusa alimvamia polo kwa matusi “Unaambia nani hivyo? Wewe ni mjinga sana. Leo ujanja wako lazima ukome. Pasta hakuna harusi itaendelea hapa. Hii mimba nimebeba hata yeye mwenyewe anajua ni miezi sita. Saa hii anajaribu kuniruka. Kwani niliipata through osmosis?” kipusa alisimama kidete.

Ilibidi harusi iahirishwe kwa muda.