Jombi adinda kulipa mahari akidai mke ni mvivu

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Monday, May 16  2016 at  12:59

Kwa Muhtasari

LUANDA, Vihiga

Kalameni kutoka eneo hili, alishangaza mashemeji wake baada ya kuwaeleza kuwa wasitarajie mahari yoyote kwa sababu dada yao alikuwa mvivu.

 

KALAMENI kutoka eneo hili, alishangaza mashemeji wake baada ya kuwaeleza kuwa wasitarajie mahari yoyote kwa sababu dada yao alikuwa mvivu.


Kulingana na mdokezi, polo alikuwa amechoshwa na safari za mara kwa mara za mashemeji nyumbani kwake wakidai mahari.


Inasemekana kuwa jamaa aliamua kuwaita nyumbani. Kulingana na mdokezi, mashemeji hao hawakukawia kwenda wakidhani aliwaitia mahari.


“Mimi nimewaita hapa ili tuweze kujadiliana mambo kadhaa,” jamaa alianza kuwambia mashemeji zake. “Ninajua ya kwamba nimekaa na msichana wenu kwa muda mrefu bila kuwaletea chochote. Nyinyi mnafikiria kuwa nimewahepa,” polo aliwaeleza mashemeji zake.

 
Kulingana na mdokezi, shemeji mmoja alisimama na kuanza kuzungumza. “Shemeji sisi hatukatai chenye unasema. Lakini mtu huleta kitu kidogo kidogo.” Duru zinasema kuwa jamaa alisimama tena na kuanza kuzungumza huku hasira zikimpanda.


“Ati kitu kidogo kidogo? Kitoke wapi? Ebu niwaulize, mlipoingia katika hili boma, mmeona ng’ombe, kondoo au mbuzi wangapi? Dada yenu kwanza ni mvivu namba one. Sasa mnataka niwape nini?” polo aliwauliza mashemeji zake.


Inasemekana kuwa mashemeji walianza kuangaliana. “Sasa unamaanisha nini?” polo mmoja alimuuliza. Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, polo na mashemeji zake walianza kurushiana cheche za matusi.

“Kila mara mnakuja hapa mkitaka mahari, please tell your sister aanze kutafuta hiyo mahari. Mtu anayelala mpaka saa tano mchana. Ninamlisha tu kama ndege. Halafu mnanisumbua hapa eti mahari. Kwendeni huko,” polo aliwazomea mashemeji zake.