Wang'ang'ania polo kama mpira wa kona mbele ya mke wake

Na GRACE KARANJA

Imepakiwa - Thursday, May 19  2016 at  12:37

Kwa Muhtasari

DANDORA, Nairobi

Kioja kilizuka mtaani hapa vipusa wawili walipomenyana vikali wakimng’ang’ania polo mbele ya mke na watoto wake.

 

KIOJA kilizuka mtaani hapa vipusa wawili walipomenyana vikali wakimng’ang’ania polo mbele ya mke na watoto wake.


Kulingana na mdokezi, wawili hao walikuwa wamealikwa na polo kuhudhuria sherehe za kuzaliwa kwa mwanawe.


Inasemekana kuwa polo hufanya biashara ya kupika na kuuza chakula na wawili hao walikuwa wateja wake lakini hawakuamini kwamba alikuwa na mke. Kila mmoja alikuwa akimmezea mate.


Siku ya kisanga wawili hao walifika kwa jamaa wakiwa wamevalia mavazi ya kisasa huku wamejipodoapodoa kwelikweli kisha wakaketi karibu na polo.


“Usiniambie hata wewe uko hapa. Mimi nitaketi karibu naye hata kama ana mke sijali,” mmoja alimwambia mwenzake.
Hapo ndipo mwenzake alisimama na bila kuona haya akaanza kumpapasa polo mkono mbele ya mkewe na mtoto.


“Naona una mke na mtoto tuliyekuja kumsherehekea lakini najua mapenzi ndiyo yalikufanya unialike. Sasa amka tuanze kula ngoma,” alimuomba polo.


Hata hivyo, polo alisimama na kuwaonya vikali dhidi ya kumharibia sherehe za mwanawe.


“Niliwaalika hapa ndio mjue kwamba nina mke na mtoto na siwezi kumwacha kwa sababu yenu, nawaheshimu kama wateja wangu lakini mengine mwajidanganya tu. Kwa sasa, ondokeni kwangu kwa sababu hamna nia nzuri,” polo aliwaonya wawili hao ambao tayari wana watoto nje ya ndoa.


Hapo ndipo walianza kukabiliana wenyewe kwa wenyewe wakilaumiana vikali. Hakuna aliyewatenganisha na mara moja, mke wa polo akawafurusha nje.


“Hamna haya, nendeni mkatafute baba za watoto hao wenu, mwacheni mume wangu,” mke wa polo aliwaonya wawili hao.