Polo arukwa na akili baada ya Sportpesa kunyonya hela zake

Na DENNIS SINYO

Imepakiwa - Friday, May 20  2016 at  16:52

Kwa Muhtasari

KABRAS, Malava

MAMA kutoka eneo hili aliwashangaza wakazi kwa kutisha kumripoti mumewe kwa polisi akidai alichanganyikiwa baada ya kupoteza pesa nyingi kwenye mchezo wa bahati nasibu katika Sportpesa.

 

MAMA kutoka eneo hili aliwashangaza wakazi kwa kutisha kumripoti mumewe kwa polisi akidai alichanganyikiwa baada ya kupoteza pesa nyingi kwenye mchezo wa bahati nasibu katika Sportpesa.

Yaarifiwa kwamba mume wa mama huyo alikuwa akishiriki kamari hiyo kila siku huku akiwa na matumaini kwamba angeshinda hela nyingi na kuishi maisha ya raha mstarehe.

Hata hivyo, jamaa huyo anasemekana kuwa mkali zaidi akikosa kushinda pesa kwenye mchezo huo. Kulingana na mdokezi, hali hii ilikuwa ikimfanya jamaa kutotulia usiku kucha huku akiamka kila mara kutazama iwapo alikuwa ametumiwa ujumbe wa kushinda kwenye simu yake.

Hali ilipoonekana kuwa mbaya zaidi, mama huyo alimjuza shemeji yake na kumuomba amshauri jamaa kuacha kushiriki michezo hiyo.

Hata hivyo, inasemekana ndugu ya jamaa aliogopa akisema kwamba jamaa hangemsikiza hata kidogo. Hali hii ilimfanya mama huyo kutisha kupiga ripoti kwa polisi kwamba mumewe alikuwa hatulii nyumbani na kukataa chakula baada ya kukosa kushinda.

Kukataa chakula

“Usiku hulali hata kidogo, kila mara ni simu tu, anapogundua kwamba hujashinda kitu, huwa na mawazo mengi sana

kukataa chakula,” alieleza mama huyo.

Ilisemekana kwamba jamaa alikuwa amepoteza pesa nyingi sana kwenye michezo hiyo ya kubashiri matokeo ya spoti ila hakuwa akibahatika kushinda kitita alichonuia.

Licha ya mkewe kumrai kuacha uraibu huo, jamaa alikuwa akimfokea na kumtaka kuachana naye kabisa.“Nimetumia njia zote kukusaidia ila nimeshindwa, sasa hii lazima ifike polisi,” mama huyo alimtisha mumewe.

Hata hivyo, wakazi walimshauri mama huyo kumtafutia jamaa ushauri nasaha aitwe kusaidiwa kuepuka majuto ya kutoshinda michezo ya bahati nasibu.

Wakazi walimlaumu vikali mama huyo kwa kumtakia mumewe mabaya kwa kutisha kumshtaki kwa polisi.