Jombi arudi ocha kusaka aliyemroga

Na TOBBIE WEKESA

Imepakiwa - Monday, May 23  2016 at  14:34

Kwa Muhtasari

CHWELE, Bungoma

Kalameni aliwashangaza wenyeji wa eneo hili aliporejea kutoka jijini kwa lengo la kumsaka mtu aliyeshuku alimroga. Inasemekana kuwa lengo la polo lilikuwa ni kumwadhibu aliyemroga.

 

KALAMENI aliwashangaza wenyeji wa eneo hili aliporejea kutoka jijini kwa lengo la kumsaka mtu aliyeshuku alimroga. Inasemekana kuwa lengo la polo lilikuwa ni kumwadhibu aliyemroga.


Kulingana na mdokezi, polo alikuwa akioa lakini hakuna mwanamke aliyeishi naye kwa muda mrefu. “Wote walikuwa wakimtoroka baada ya muda mfupi,” alieleza mdokezi. Inasemekana kuwa jambo hili lilimkasirisha polo hadi akaamua kuhamia jijini.


“Kwani mimi nina shida gani? Watoto wa juzi wameoa na wanaishi na wake zao vizuri. Lazima kuna mtu anayeniangalia na jicho baya,” polo alisema.


Duru zinasema kwamba polo alipofika jijini, alimpata kipusa mwingine ambaye walioana lakini pia hawakuishi kwa muda mrefu.


Inasemekana kuwa polo alipokuwa anarejea kwake wakati wa jioni kutoka kazini, aliona kibango ambacho kilikuwa na maandishi yasemayo mganga wa kulinda ndoa.


Duru zinasema kuwa polo aliamua kumtembelea mganga huyo akiwa na matumaini ya kupata suluhisho la tatizo lake. Inasemekana kuwa mganga alimfichulia polo mtu aliyemfanya asiishi na mke.

“Wazee wananiambia kuwa wewe ulifungwa. Hakuna mke atakayeishi na wewe. Aliyekufunga ni jirani yako,” mganga alimueleza polo.


Kulingana na mdokezi, polo alitoka kwa mganga akiwa na hasira na kuelekea moja kwa moja hadi kwao kijijini kumsaka mtu aliyetajwa na mganga,” alieleza mdokezi.


Inasemekana kuwa alipofika kijijini, polo alielekea kwa wazazi wake ambapo aliwaeleza shughuli iliyomleta. “Mimi nimekuja kumtafuta mtu asiyenitakia mazuri. Nimetoka kwa mganga na akaniamba kuwa ni jirani yetu ndiye ananiroga. Lazima nimwadhibu leo,” polo aliwaeleza wazazi wake.


“Umehadaiwa bure na mganga, jirani yetu si mchawi,” polo alielezwa na wazazi.